Mbunge wa CUF amponza wa Chadema, atimuliwa bungeni

Mbunge wa Mlimba (Chadema), Susan Kiwanga

Muktasari:

Uvumi wa kujiuzulu kwa mbunge wa Tandahimba (CUF), Ahmed Katani imempongeza mbunge wa Mlimba (Chadema), Susan Kiwanga kufukuzwa bungeni na Spika Ndugai hadi Januari mwakani.

Dodoma. Spika wa Bunge, Job Ndugai amemfukuza bungeni Mbunge wa Mlimba (Chadema), Susan Kiwanga (Chadema) kwa kile alichodai ni utovu wa nidhamu.

Spika Ndugai amefikia uamuzi huo baada ya kukaa kwa muda akitaka vyombo vimsaidie kumpata mbunge aliyefanya utovu wa nidhamu wakati mbunge wa Tandahimba (CUF) Katani Ahmed Katani alipokuwa akitoa mchango wake.

Katani ameanza kwa kukanusha madai ya kujiuzulu akisema vyombo vya habari havikumtendea haki ndipo wabunge wa upinzani wakaanza kupiga kelele lakini Spika alipowanyamazisha wakaanza kuzomea.

"Nimejiridhisha kupitia vyombo vyangu, aliyefanya utovu wa nidhamu ni mheshimiwa Susan Kiwanga, sasa nakuomba utoke nje hadi bunge lijalo tutaonana Mungu akipenda Januari mwishoni mwakani," amesema Spika Ndugai

Amemtaka mbunge huyo kutojihusisha na vikao au kamati za Bunge katika kipindi hiki na kuwa kama alikuwa kwenye orodha ya wachezaji wa Bunge anapaswa kuondolewa jina lake.

Katika mkutano wa 13 huyu anakuwa mbunge wa pili kufukuzwa baada ya jana Jumatano Mbunge wa Iringa Mjini (Chaden) Mchungaji Peter Msigwa kufukuzwa na Naibu Spika Dk Tulia Akson baada ya kuambiwa alikuwa anapiga kelele.