Mchina mahakamani kwa tuhuma za kutaka kumpa rushwa RC Geita

Muktasari:

Mfanyabiashara wa madini raia wa China amefikishwa  mahakamani na Takukuru  kwa kosa la kushawishi na kujaribu kutoa rushwa kinyume na kifungu cha 15(1)(b) cha sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007.  

Geita. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Geita imemfikisha mahakamani raia wa China kwa kosa la kumshawishi mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel ili ampe rushwa ya Sh1milioni.

Katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo Ijumaa Desemba 7, 2018 na Mkuu wa taasisi hiyo mkoani Geita, Thobias Ndaro inasema mshtakiwa huyo,  Cheng Li  ni mfanyabiashara wa madini.

Inaeleza kuwa alifikishwa mahakamani jana Novemba 6, 2018 mbele ya hakimu mfawidhi wa mahakama ya Hakimu Mkazi Geita,  Jovith Kato.

Akisoma mashtaka mwendesha  mashtaka wa Takukuru, Dennis Lekayo amedai mahakamani hapo kuwa Oktoba na Novemba, 2018 mshtakiwa  alimshawishi Gabriel kwa njia ya ujumbe wa simu akitaka kumpatia Sh1milioni kila mwezi.

Ilielezwa mahakamani hapo kuwa katika kuonyesha amedhamiria kutoa rushwa alituma ujumbe mwingine akimshawishi kumpelekea kiasi hicho cha fedha  na majani ya chai kutoka China.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa baada ya ujumbe huo, mkuu huyo wa mkoa alitoa taarifa Takukuru ambao waliweka mtego uliofanikisha kumkamata mshtakiwa akiwa ofisini kwa Gabriel akijiandaa kutoa rushwa ya Sh1milioni na majani hayo ya chai.

Mshtakiwa  amekwama makosa na yuko nje kwa dhamana huku kesi hiyo ikiahirishwa hadi Desemba 20, 2018.