Mchungaji Mashimo alitimuliwa kanisani kisa Wema Sepetu

Jina la mchungaji wa Mitume na Manabii, Daudi Mashimo limekuwa maarufu kwa ghafla baada ya kuhusika katika kumtolea dhamana msanii Rutyfiya Abubakary maarufu kama ‘Amber Ruty’.

Mashimo amekuwa gumzo mitandaoni na mara kwa mara ameonekana akitangaza kumfanyia maombi Miss Tanzania wa 2006 na mwigizaji bora wa mwaka, Wema Sepetu.

Juzi alifanya mahojiano na Mwananchi na kuzungumza mengi ikiwamo kujitambulisha na kueleza sababu za kufanya mambo yanayolifanya jina lake kuwa gumzo.

Moja ya mikasa aliyokumbana nayo hivi karibuni ni kutimuliwa katika kanisa alilokuwa akihudumia baada ya kutangaza kufanya maombi maalumu kwa ajili ya Wema Sepetu ambaye hivi karibuni aliingia matatani akituhumiwa kuchapisha picha zisizo na maadili mtandaoni.

Anasema baada ya kutangaza ibada maalumu aliambiwa achague moja, kuachana na hilo au aondolewe kanisani, naye alichagua moja kuendelea na maombi ya Wema Sepetu.

Anasema kutokana na hilo sasa anasali chini ya mti alipojisitiri kwa kuweka maturubai huku waumini wakipungua kutoka 80 na kufika 30.

“Nilipanga kufanya maombi kwa ajili ya Wema lakini nikapigwa vita na wenzangu, niliamua kuondoka kwa kuwa tayari nilikuwa na maono,” anasema.

Amber Ruty alimuona mara ya kwanza Gerezani

Anasema kwamba licha ya kujifunga na kuamua kwenfa kumuwekea dhamana Amber Ruty, hakuwa akimjua dada huyo na mara ya kwanza kuonana naye ni gerezani alipokwenda kumtembelea.

Anasema kilichomvuta kwenda kumuona ni kutokana na kupata maono juu yake kwamba ni lazima amtoe mahabusu na yeye kulazimika kuyatekeleza maagizo hayo ya Mungu Novemba 26, mwaka huu na tayari ameonyesha kuwa tayari kuokoka yeye na mpenzi wake.

“Nilikwenda gerezani mara tatu kuonana na Amber Rutty na mpenzi wake Said, niliwaambia lazima mtoke,” anasema.

Kuhusu kesi inayowakabili anasema kwamba hata yeye amesikia kuhusu suala la video lakini hajawahi kuziona.

Anahubiri stendi kila siku

Ingawa alikuwa na nyumba ya kufanyia Ibada, lakini mchungaji huyu anasema kila siku lazima afike katika stendi ya Mbezi mwisho kuombea watu hasa wasafiri ili kuwaepusha na ajali.

Anasema kazi hii huifanya kuanzia saa 10.00 alfajiri hadi saa 4.00 asubuhi kabla ya kwenda katika shughuli nyingine na kuongeza kuwa kila siku si chini ya watu wanane hadi 10 wamekuwa wakiokoka kutokana na mahubiri yake.

“Mwanzo nilipokuwa nikifanya huduma hii, watu walikuwa wakiokoka kwa kukubali kile nilichokuwa nikihubiri, mwisho nikasema sasa hawa baada ya hapa wanaenda wapi, ndipo hapo nilipopata wazo la kuwa na kanisa.

Mchungaji Mashimo anasema kila siku hulala saa tatu tu, zilizobaki huzigawa katika kufanya maombi, mazoezi, shughuli za kujiingizia riziki na nyinginezo.

Mama yake ni mganga wa kienyeji

Mashimo ni mtoto wa saba kati ya watoto sita wa familia ya Mzee Mashimo Nkuba.

Baba yake akiwa mfanyabiashara wa madini, anasema mama yake mzazi ni mganga wa kienyeji.

Anasema pamoja na mama yake kuwa mganga anamuheshimu kadri inavyotakiwa lakini linapokuja suala la Mungu huwa anakuwa adui na huwa anamweleza mara kwa mara.

Auza mitumba, kuchimba madini

Katika harakati za kutafuta maisha, Mchungaji Mashimo anasema alishafanya kazi mbalimbali ikiwemo kuuza mitumba kazi ambayo alikuwa akiifanya katika Kituo cha Bakhresa maeneo ya Tazara Jijini Dar es Salaam.

Pia, aliwahi kufanya biashara ya madini kazi ambayo alirithi kutoka katika familia kwani mbali na baba yao kumiliki baadhi ya mashimo katika migodi mbalimbali mkoani Simiyu, baadhi ya ndugu zake nao wamekuwa wakiifanya kazi hiyo.

Hata hivyo, anasema ilifika mahali kazi hiyo ikamshinda kutokana na mambo aliyoyakuta ndani yake ndipo alipoamua kuingia katika shughuli za mahubiri.

Mwigizaji wa filamu, mcheza kareti, ngumi

Anasema ilipofika mwaka 2002 alikutana na aliyekuwa Mwenyekiti wa Shirikisho la Wasanii (SHIWATA), Mwalimu Twaalib, (sasa ni marehemu) ambaye pia alikuwa akimiliki chuo cha kufundisha filamu ambaye alimsaidia kumsomesha masuala ya filamu.

Akiwa huko anasema aliweza kukutana na wasanii mbalimbali akiwamo Chiki Mchoma ambaye alimuunganisha na hatimaye kuingia katika kikundi cha maagizo cha Kaole.

Akiwa na kikundi cha Kaole alicheza michezo mbalimbali ukiwamo wa ‘Tetemo’ kama askari wa kituo cha kulelea watoto yatima.

Mchungaji huyo anasema kwamba baadaye aliachana na kikundi hicho na kujiunga na kampuni ya filamu ya Simple Production, iliyokuwa ikimilikiwa na msanii Kevin na Nikita.

Akiwa katika kampuni hiyo alicheza filamu mbalimbali ikiwamo ya Dangers Father kama askari, Well Done My Son sehemu ya kwanza hadi ya tatu kama askari wa Nikita.

Anasema nafasi za kuwa askari zilionekana kumfaa zaidi kutokana na kuwahi kijifunza mchezo wa ngumi na kareti, hivyo anapokuwa anaigiza huuvaa uhalisia vizuri tofauti na mtu ambaye hajapitia huko.

Filamu nyingine alizocheza ni ‘Wageni Wangu’ na ‘Ndoa yangu ‘aliyoshirikishwa na msanii Jacob Steven maarufu kama JB ambapo anasema mpaka sasa jumla ya filamu alizowahi kucheza hazipungui 15. Katika kujitanua kisanaa, anasema kwamba baadaye aliamua kufungua kampuni aliyoipa jina la Mwamba Arts ambayo mbali na kutengeza filamu pia alikuwa akimiliki wasanii zaidi ya 980 wakiwa katika mikoa minne nchini.“Nadhani mimi ndiye msanii wa kwanza kumiliki wasanii wengi kwa wakati mmoja na wakiwa kambini niliweza kuwahudumia kuanzia chakula cha asubuhi, mchana na jioni bila ubabaishaji kama wanavyofanya wengine na bado niliwalipa ujira wao,” anasema Mashimo.

Kupitia kampuni yake hiyo anasema alitengeneza filamu mbili ikiwamo ‘Dengue na ‘Uchungu wa Mwana’ na sasa yupo katika harakati za kuachia filamu nyingine ya ‘Begi la Mchungaji’ na ‘Nabii wa Sasa’, ambazo zitaelezea yaliyo nyuma ya viongozi wa dini.

Humwambii kitu kwa Gwajima, Moses Kulola

Katika kila kazi ambayo mtu amekuwa akiifanya lazima kuna mtu ambaye anakuwa amemvutia kuingia katika kazi au taaluma hiyo, Mashimo yeye anasema kwamba waliomvutia kufanya kazi ya uchungaji ni Askofu Josephat Gwajima wa Kanisa la Ufufuo na Uzima.

Mwingine aliyemtaja ni aliyekuwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Asemblies Of God (EAGT), Askofu Moses Kulola ambaye alifariki dunia mwaka 2013.

Mashimo anafafanua kwamba sababu ya yeye kuwapenda wachungaji hao na kutamani kufuata nyayo zao ni kutokana na kuwa viongozi wa dini wa kweli huku akitamani roho aliyokuwa nayo Kulola kungekuwa na uwezo ingeoteshwa kwake.