Membe njiapanda

Dar es Salaam. Mwaka 2014, Bernard Membe na wanachama wengine watano walifungiwa kwa miezi 12 baada ya kubainika kuwa walikuwa wakifanya kampeni kabla ya muda.

Walitumikia adhabu hiyo hadi mwisho na muda ulipofika, wote walichukua fomu za kuomba kupitishwa na CCM kugombea urais. Wote hawakupita, lakini ni Membe aliyeishia hatua ya tano bora.

Miaka minne baadaye, Membe, ambaye alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje kwa miaka takriban nane katika Serikali iliyopita, anakabiliwa na mazingira kama hayo.

Safari hii Membe ameitwa ofisini kwa katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally akitakiwa ajieleze dhidi ya tuhuma za kupanga mkakati wa kumkwamisha Rais John Magufuli kumalizia kipindi cha miaka mitano, na kuanza mikutano ya harakati za kujitosa katika mbio za urais 2020.

Tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu 2015, mbunge huyo wa zamani wa Mtama amekuwa kimya na huonekana mara chache katika shughuli za kijamii, lakini hiyo haijamuepusha dhidi ya tuhuma hizo zilizoibua mijadala.

Akizungumza na wanachama wa CCM mkoani Geita kuhusu umuhimu wa mshikamano, Dk Bashiru alisema ameshazungumza na wanachama wote waliotaka urais mwaka 2015 isipokuwa Membe, ambaye amekuwa akisikia habari zake kuwa anaandaa mkakati wa kugombea urais mwaka 2020 na kufanya mipango ya kumkwamisha Rais Magufuli.

Dk Bashiru, ambaye alikosolewa na katibu wa zamani, Pius Msekwa kwa kitendo hicho, alimtaka Membe afike ofisini kwake.

Akaunti ya Twitter iliyokuwa na jina la Bernard Membe ilimjibu kuwa imeitikia wito huo na kuweka sharti kuwa siku atakayokwenda awepo na mtu aliyetoa tuhuma hizo ili aweze kuzithibitisha.

Baadaye CCM ilifunga mjadala huo, lakini wito wa Dk Bashiru kwa Membe haujafutwa na hivyo mwanadiplomasia huyo, ambaye alikuwa nje ya nchi wakati wa malumbano hayo, anajiandaa kwa kikao hicho ambacho kinaweza kuamua hatima yake kama ilivyokuwa mwaka 2014 au adhabu ikawa kubwa zaidi .

Pamoja na Membe wengine waliotiwa hatiani mwaka 2014 ni mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye, mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja na mawaziri wengine wawili, January Makamba (Sayansi, Teknolojia na Mawasiliano) na Steven Wasira (Uhusiano na Uratibu).

Membe anaweza kumshawishi Dk Bashiru kuwa hahusiki na wala hana mipango hiyo, hali itakayomfanya mtendaji huyo mkuu wa CCM kutafuta ushahidi.

Ikiwa mazungumzo ya Membe na Dk Bashiru yatachukua picha kubwa, huenda kada huyo akapelekwa Kamati ya Maadili, ambayo ilimuadhibu na wenzake watano mwaka 2014. Hatua hiyo itamweka njiapanda mshauri huyo wa zamani wa masuala ya usalama.

Wadau waliotakiwa na Mwananchi kutoa maoni yao kuhusu mkutano wa Membe na Dk Bashiru walikuwa na maoni tofauti.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Taifa, Erasto Sima alisema wito ni wito, uwe umetolewa kwa barua au kwa simu ili mradi uwe umetolewa na kiongozi mkuu wa chama.

“Mwanachama yeyote anayekiuka wito wa viongozi hatua ya kwanza ni kupelekwa kwenye kamati ya maadili,” alisema Sima.

Aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema masuala ya ndani ya chama yanapaswa kumalizwa na wanachama wenyewe.

“Chama cha siasa ni umoja wa watu wenye msimamo mmoja hivyo wanao utaratibu wa kurekebisha endapo mmoja kati yao atakiuka makubaliano au msimamo uliopo,” alisema mwanaharakati huyo.

Hata hivyo, alisema utaratibu alioutumia Dk Bashiru kumuita Membe hadharani si wa kiungwana na anaweza asiutekeleze kwani kuna akina Membe wengi nchini hivyo hakuna anayepaswa kuamini kuwa anayeitwa ni yeye.

Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde alisema ni mapema sana kujua uamuzi utakaotolewa na Dk Bashiru kwani hajaweka wazi lengo la wito huo.

“Katibu mkuu anaongoza wanachama. Ana haki ya kumuita na kuzungumza na mwanachama yeyote wa chama chetu,” alisema.