Meya Dar aamuru polisi wenye silaha kutoka ukumbini

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani la Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita amewaamuru polisi wenye silaha za moto waliokuwa ndani ya ukumbi wa mkutano kutoka nje kwa madai uwapo wao unawatisha wajumbe.

Dar es Salaam. Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita amewataka polisi wenye silaha za moto kutoka nje ya ukumbi wa Baraza la Madiwani wa jiji hilo kwa madai kuwa uwapo wao unawatisha wajumbe wa baraza hilo.

Mwita alitoa amri hiyo leo baada ya mmoja wa wajumbe wa baraza hilo, Saed Kubenea kuomba utaratibu kuhusu uwapo wa askari na uhuru wa kutoa maoni.

Ilivyokuwa

Baada ya dua ya kuliombea baraza hilo lenye ajenda ya uchaguzi wa Naibu Meya wa jiji ili kuziba nafasi ya Mussa Kafana aliyejiuzulu na kuhamia CCM, Kubenea alisema: “leo mkutano huu una wageni wengi hasa askari polisi wenye silaha za moto tena ndani ya ukumbi lakini siyo utaratibu mwenyekiti.”

"Hatukatai vyombo vya usalama kuwapo humu ndani lakini hizi silaha za moto si sahihi. Tunaomba watoke nje ili tuendelee na kikao.”

Baada ya maelezo hayo, Mwita alimpa nafasi katibu wa baraza hilo, Sipora Liana kutoa ufafanuzi kuhusu hatua ya polisi wenye silaha kuwapo ndani ya kikao hicho.

"Mimi ndiye nimeandaa mkutano huu, nimeamua kuweka ulinzi kutokana na historia ya vikao vya nyuma kuwa na vurugu. Nataka mkutano uwe na ulinzi na utulivu.”

"Nimewahakikishia ulinzi wajumbe wangu ndiyo maana ulinzi upo hapa nami ndio muandaaji wa kikao hiki,” alisema Liana.

Baada ya maelezo hayo, Mwita alimpa nafasi tena Kubenea ambaye alsisitiza polisi hao watoke nje na kama vurugu zitatokea  wataitwa ndani.

“Hata kule bungeni vurugu zikitokea Spika ana agiza askari waingie ndani," alisema Kubenea.

Maelezo hayo ya Kubenea yalimfanya Mwita kuagiza askari waliokuwa na silaha watoke nje ya ukumbi jambo ambalo lilitekelezwa.

Wakati Meya wa Ubungo akisikika akisema hatoweza kutoa maoni huku askari hao wakiwa ukumbini na silaha, mjumbe mwingine wa CCM, Mussa Ntinika alisikika akisema siyo jambo jema na halileti tafsiri nzuri kwa vyombo vya ulinzi kutolewa nje ya ukumbi.