UCHOKOZI WA EDO: Mheshimiwa angetoa hotuba hii 2015 nisingefunga duka

Mheshimiwa namba moja wa nchi hii, akisisitiza kitu kwa lugha ya Kiingereza ujue kimemuumiza sana. Juzi nilimsikia katika hotuba yake ya mambo ya kodi akitoa kitu moyoni. Alitumia Kiingereza kusisitiza kuhusu makusanyo ya kodi. Alisema, “we are very poor.” Akimaanisha katika makusanyo ya kodi.

Baadaye akamwaga nondo nzito. Utakuwa mchawi kama hukumwelewa alichokuwa anasema. Aliweka wazi kuwa TRA na Polisi wananyanyasa wafanyabiashara. Mimi nikiwa mmoja wapo hata kama sifanani na Rostam Aziz au Mzee Bakhresa.

Namba moja aliongea kwa hisia kali mpaka nikakumbuka fremu yangu niliyoifunga Desemba 2015. Miezi miwili tu baada ya yeye kuingia madarakani. Kama hotuba yake ya juzi angeitoa wakati huo nadhani nisingefunga.

Hotuba za wakati ule zilikuwa katika msisitizo huu huu, lakini dhidi ya wafanyabiashara, za leo ni dhidi ya TRA na Polisi. Zile za wakati ule kama mheshimiwa angesoma picha halisi angegundua kwamba wafanyabiashara walikuwa tayari kulipa kodi na sio wezi.

Tatizo nadhani kuna watu walimdanganya kwamba wafanyabiashara wote ni wezi na hawataki kulipa kodi. Hapana, ukweli ni ule aliousema juzi. Kuna kodi za kubambikiwa, zingine za kukomoana. Hazilipiki.

Wakati ule alipaswa kusimama katikati na kuweka sawa majadiliano kati ya mamlaka dhidi ya wafanyabiashara. Kifo cha biashara ni msiba kwa Serikali na mfanyabiashara. Tatizo awali ilidhaniwa kwamba ni msiba kwa mfanyabiashara tu. Imechukua muda mrefu kugundua ni msiba wa wote.

Mimi na wenzangu tulifunga fremu zetu na watu wakashangilia kwa kudhani waathirika ni sisi tu, kumbe ni wote. Nashukuru namba moja amegundua na sasa naweza kufungua kibanda changu. Siwezi kusema kipo wapi kwa sababu najua bado kuna watoza kodi hawajamwelewa vema na sisi tunaojulikana ndio tunakuwa wahanga wakubwa zaidi. Mabwana kodi wanapishana katika fremu kutoza kodi kama abiria wanavyopishana katika mlango wa Daladala. Namba moja nadhani pia amegundua majadiliano kati ya washika virungu na wanaokimbizwa ni kitu muhimu ili kufikia malengo. Naenda kufungua kibanda changu. Mama mwenye nyumba alijaribu kupangisha kwa wengine lakini ilishindikana. Nani alitaka kodi za kukomoana?