Miradi mikubwa kielelezo cha misimamo ya Magufuli

Muktasari:

Unahitaji kuwa na hoja zenye nguvu na ushawishi wa hali ya juu kuweza kubadili msimamo wa Rais John Magufuli kuhusu kitu ambacho anakiamini baada ya kukifanyia utafiti na kujiridhisha.


Unahitaji kuwa na hoja zenye nguvu na ushawishi wa hali ya juu kuweza kubadili msimamo wa Rais John Magufuli kuhusu kitu ambacho anakiamini baada ya kukifanyia utafiti na kujiridhisha.

Na hoja zako zikiwa hazina nguvu na hazijamridhisha, atasimama jukwaani kukuaibisha, kama ilivyokuwa kwa wale waliopewa jukumu la kufanya tathmini ya athari za mazingira kuhusu mpango wa kujenga mradi wa kuzalisha umeme katika korongo la Stiegler, maarufu kama Stiegler’s Gorge mkoani Morogoro.

Na ndivyo anavyofanya kwa wengine wote wanaopinga mipango aliyopanga kuitekeleza katika kipindi chake cha kwanza cha miaka mitano ya urais kinachoisha mwaka 2020, akitegemewa kusimama tena jukwaani kuomba kura za wananchi ili wamruhusu arudi tena Ikulu kwa miaka mingine mitano.

Mfano mkubwa wa jinsi Rais Magufuli asivyobadili msimamo wake kirahisi ni mradi huo wa umeme, lakini amefanya hivyo katika miradi mingine mikubwa anayoendelea kuitekeleza na ambayo yote imekosolewa vikali na wadau kwa sababu tofauti; uharibifu wa mazingira, mradi kutokuwa kipaumbele cha nchi kwa sasa, kutopata baraka za Bunge na sababu nyinginezo.

“Inyeshe mvua, lije jua, mradi wa umeme wa Stieglers Gorge lazima ujengwe,” alisema Rais katika moja ya hotuba zake. “Hatutawasikiliza watu ambao wanazungumzia athari za mazingira bila ya kuwa na ushahidi.”

Alikuwa akizungumzia moja ya miradi ambayo ameanza utekelezaji wake ndani ya miaka mitatu ya uongozi wake tangu aliposhinda uchaguzi wa Rais mwaka 2015 na kuapishwa Novemba 5 mwaka huo.

Mradi ulioibua mjadala mkubwa ni wa kujenga kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia mashine zinazoendeshwa kwa maji (Stiegler’s Gorge Hydroelectric Power Station) ambao ukikamilika utakuwa ukizalisha megawti 2,100 au 5,920GWh kwa mwaka.

Mradi huo utajengwa katika Hifadhi ya Selous mkoani Morogoro. Eneo la mradi huo (kilomita 1,350 za mraba) katikati ya moja ya hifadhi kubwa duniani, limesababisha mjadala mkubwa kuhusu mazingira, baadhi wakisema kuwa ukubwa wa eneo ambalo miti itakakatwa kupisha mradi huo unalingana na mkoa wa Dar es Salaam hivyo utaathiri si tu wanyama walioko Selous, bali viumbe wengine wanaoishi kutegemea Mto Rufiji na huduma za ekolojia zinazotokana na mto huo.

“Kwanza, ni asilimia 3.5 ya eneo lote la hifadhi ndiko kutajengwa mradi wa umeme. Hata hivyo, wanyama watapata maji ya kunywa ya kutosha,” alisema Rais akijibu wakosoaji wa mradi.

Kati ya taasisi zinazopinga utekelezwa wa mradi huo ni Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu Sayansi na Utamaduni (Unesco) ambalo limeiweka hifadhi hiyo katika urithi wa dunia, na Mfuko wa Kimataifa wa Wanyamapori (WWF) ambao walisisitiza kuwa athari hizo katika ripoti yake ya utafiti iliyotolewa mwaka jana.

Lakini Rais Magufuli, ambaye ameahidi uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 kwa kutegemea viwanda, amesimamia msimamo wake wa kujenga mradi huo, na hasa faida zake katika uchumi wa viwanda.

Ujio wa treni ya umeme inayojengwa sambamba na reli ya kati, ujenzi wa viwanda kuanzia vidogo, na shughuli nyingine za kibiashara zinazohitaji umeme wa uhakika ni moja ya sababu zinazomsukuma Rais Magufuli kuendelea na mradi huo utakaokuwa mkubwa kuliko yote ya umeme.

Na ili kuonyesha nia yake ya kufanikisha mradi huo, Serikali ya Rais Magufuli imechukua hatua kadhaa kufanikisha hilo.

Agosti 30, Serikali ilitangaza zabuni ya ujenzi wa mradi huo. Kampuni 81 zimejitokeza kununua nyaraka za zabuni ya mradi huo ambao mwaka huu umepangiwa takriban asilimia 40 ya bajeti ya 2018/19.

Mradi huo unatarajiwa kugharimu zaidi ya Sh4.5 trilioni na Rais amesema fedha za utekelezaji zipo na kudokeza kuwa ukikamilika unaweza kuitwa “Nyerere Gorge au Mwitongo Gorge”.

Treni ya pili Afrika kwa kasi

Msimamo huo wa Magufuli pia umejionyesha katika ujenzi wa reli ya kisasa (Standard gauge) na ujio na treni ya umeme ambayo anaisimamia kwa karibu. Awamu ya kwanza ya mradi huo ambayo ni kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro na ambayo utekelezaji wake umefikia asilimia 28, inatarajiwa kukamilika Novemba mwakani. Mradi huo utagharimu Sh2.7 trilioni.

Treni hiyo itakuwa ikienda kwa kasi ya kilomita 160 kwa saa na Tanzania itakuwa nchi ya pili Afrika kwa treni yake kuwa ya kasi zaidi. Ya kwanza ni Morocco.

Awamu hiyo yenye urefu wa kilomita 205 za njia kuu na 95 za kupishania treni, inajengwa na kampuni za Yapi Merkenzi Instant Ve Sanayi A.S ya Uturuki na Mota-Engil, Engenharia E and Construcao S.A ya Ureno,

Reli hiyo ya kisasa itakuwa na uwezo wa kusafirisha mizigo ya uzito wa tani milioni 17 ikiwa ni ongezeko la karibu mara mbili na nusu ya uzani wa awali.

Mradi huo kwa ujumla una awamu tano na ukikamilika utarahisisha usafiri wa abiria na mizigo kati ya Tanzania, Rwanda na Burundi, ukichangamsha zaidi kiuchumi wananchi wanaoishi mikoa ambayo reli imepitia.

ATCL na asilimia 24 ya soko

Pengine mradi mwingine uliokosolewa sana ni wa kufufua Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), ambao umehusisha ununuzi wa ndege saba tatu zikiwa zimeshafika na kuanza kufanya safari za ndani na kulifanya shirika hilo kukamata asilimia 24 ya soko tofauti na awali lilipokuwa na asilimia 2.

Magufuli alianza kwa kununua ndege mbili aina ya Bomberdier Q400 ikiwa ni takribani miezi 10 tangu aapishwe na hapo ndipo ATCL ilipoanza kuinua kichwa kwa kuanzisha safari kadhaa za mikoani.

Mwanzoni mwa mwaka huu iliwasili ndege nyingine aina ya Q400 na kufanya jumla ya ndege za aina hiyo kuwa tatu, kabla ya kuwasili kwa ndege kubwa ya Boeing 787-8 (Dreamliner) Julai mwaka huu. Ndege nyingine mbili aina ya Airbus A220-300 zitawasili Desemba na Dreamliner nyingine ikitarajiwa mwakani.

ATCL ambayo inatarajia kuanza kupata faida ifikapo 2023, sasa inasafiri katika mikoa 12, inatarajiwa kuanza safari za Burundi na Uganda na huku ikiendelea kwenda visiwa vya Comoro. Dreamliner inatarajiwa kufanya safari za Mumbai, India na Guangzhuo, China.

Shirika hilo sasa limefanikiwa kuongeza mapato ya kila mwezi kufikia Sh4.5 bilioni kwa mwezi mwaka 2017 tofauti na mwaka 2016 ambapo mapato yake yalikuwa Sh700 milioni kwa mwezi.

Kiwango cha hasara nacho kimepungua kutoka Sh14.2 bilioni mwaka 2016 hadi Sh4.3 bilioni mwaka 2017. Lakini mradi huo unapingwa na wakosoaji wanaosema ndege hizo hazikuwa muhimu kwa sasa kwa kuwa Watanzania wengi wanatumia usafiri wa mabasi, reli na meli na hivyo hawaoni umuhimu wa ndege.

Lakini Magufuli amewapinga kwa kusema huwezi kujenga uchumi wa viwanda wakati huna ndege na kwamba suala la utalii litaimarika zaidi kwa kuwa na ndege zetu za kuwabeba.

Ujenzi wa bomba la mafuta

Mradi unaoweza kuonekana kuwa ulipokelewa kwa shangwe ni ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga ambao ulizinduliwa Agosti 5, 2017. Shangwe za mradi huo zinatokana na ukweli kwamba utaajiri takriban watu 2,000 wa moja kwa moja na wengine 15,000 watakaopata fursa kutokana na ujenzi huo.

Bomba hilo lenye urefu wa kilomita 1,450 litapita mikoa minane (Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga), vijiji 184, wilaya 24 na utagharimu Sh8 trilioni.

Sababu ya pili ya kushangiliwa kwa mradi huo ni maamuzi ya haraka ya Serikali yaliyoisababisha Uganda iiengue Kenya.

Pia, Julai 2, ulifanyika uzinduzi wa mradi wa uboreshaji wa bandari ambao ulitiwa saini Juni 10, ambapo gharama za mradi huo unaotekelezwa na kampuni ya China Harbor Engineering Company (CHEC) ni Sh336 bilioni ambazo ni mkopo kutoka Benki ya Dunia (WB) na wadau wengine. Mradi huo utakamilika baada ya miezi 36.

Miradi mingine ni ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Chato uliogharimu Sh39.16 bilioni, barabara za juu katika makutano ya barabara za Nyerere na Mandela eneo la Tazara (Sh95 bilioni), makutano ya barabara za Mandela na Morogoro eneo la Ubungo (interchange) Sh188.1 bilioni na barabara nyingine ya juu katika makutano ya barabara za Nyerere na Chang’ombe, daraja la Selander linalounganisha eneo la Aga Khan na Coco Beach (Sh250 bilioni).