Mitandao ya kijamii yaivuruga CCM

Muktasari:

CCM kimewataka wananchi kutotumia vibaya mitandao ya kijamii, huku kikikanusha taarifa zilizosambaa katika mitandao hiyo zikimnukuu Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Bashiru Ally kumjibu aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.


Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimewaonya watu wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii kuweka habari za uongo zinazowahusu viongozi wa chama hicho tawala.

Pia, kimesema Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Bashiru Ally hana akaunti ya mtandao wa kijamii wa Twitter.

Chama hicho tawala kimetoa taarifa yenye ufafanuzi huo leo Jumatano Desemba 5, 2018 ikiwa ni siku moja tangu Dk Bashiru Ally kuzungumza na Mwananchi na kukanusha taarifa za mtandaoni zilizomnukuu akimjibu aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.

Taarifa hiyo iliyotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole inaeleza kuwa watu wanaotumia vibaya mitandao ya jamii wana lengo la kuleta taharuki.

“Kuna akaunti ya mtandao wa Twitter yenye jina la Bashiru Ally na inatoa kauli ambazo sio zake,” inaeleza taarifa hiyo.

“Jana katika mitandao ya kijamii watu wenye hila, fitna, husuda na kila chembe ya uzandiki wametengeneza kauli ya kubeza, potofu na isiyo na ukweli kuwa Bashiru Ally amemjibu kiongozi mstaafu, mwanachama wa CCM na kada mwenzetu mzee Pius Msekwa,” imeongeza.

Juzi Msekwa, makamu mwenyekiti wa zamani wa CCM, alizungumza na Mwananchi na kukosoa hatua iliyochukuliwa na Dk Bashiru kumwita Membe kupitia mkutano wa hadhara na badala yake akashauri atumie simu au barua.

Mbali na hayo, Polepole amesema kulikuwa na upotoshwaji wa taarifa za chama hicho iliyodai kuwepo kwa mkutano wa wanahabari katika ofisi ndogo za makao makuu ya CCM Lumumba Dar es Salaam.

“Utaratibu wa CCM msemaji ni mmoja naye ni mwenyekiti, kwa niaba ya chama anayekasimiwa dhamana ya kusema ni Katibu wa halmashauri kuu ya Taifa, mwenye dhamana ya itikadi na uenezi na si vinginevyo,” amesema Polepole.

Polepole amezitaka mamlaka zinazohusika kuchunguza na kuchukua hatua zinazostahili kwa watu wanaotumia vibaya mitandao ya jamii.