Mkurugenzi wa zamani Sikonge mbaroni kwa utapeli

Muktasari:

Polisi mkoani Dodoma wanamshikilia  Simon Ngutunga,  aliyekuwa mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Sikonge kwa tuhuma za utapeli.


Dodoma. Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma limewakamata watu wawili akiwemo,  Simon Ngatunga aliyewahi kuwa mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Sikonge mkoani kwa tuhuma za utapeli.

Akizungumza leo Ijumaa Desemba 7, 2018 Kamanda wa polisi mkoani humo, Gilles Muroto amesema kilichomponza Ngatunba ni kutaka kumfanyia mpango Razin Katundu (29) mkazi wa Yombo Buza Dar es Salaam ili apangiwe kazi Ofisi ya Rais (Tamisemi) idara ya elimu.

Amesema Katundu alikamatwa kutokana na kitendo chake cha kutaka kusaidiwa na Ngatunga ili amfanyie mpango apangiwe kazi katika idara ya elimu.

"Huyu Ngatunga anatajwa kuwa kila wakati amekuwa akijishughulisha na utapeli na anashinda Tamisemi akizurura na kuwatapeli watu kwamba atawafanyia mipango ya kazi," amesema Muroto.

Katika hatua nyingine Polisi inamshikilia Salum Pwao (31) mkazi wa Tabata kwa kujifanya ofisa wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) anayeshughulikia mafao ya wastaafu.

Amesema Pwao amekuwa na tabia ya kuwapigia simu wastaafu wanaofuatilia mafao yao na kuwadai fedha kwa ajili ya kuwasaidia ili mafao yao yatoke haraka huku wakiwadanganya kuwa mafaili yao yapo mezani kwake.

Mwingine aliyekamatwa ni Yona Julias (32) mkazi wa Dar es Salaam kwa kupitia kampuni yake anayoimiliki ya Vijana Kwanza Project inayojihusisha na upimaji wa viwanja  huku  Sham Jibrea (35)  na Meck Maula (40) wakikamatwa na misokoto 40 ya bangi.