RIPOTI MAALUM: Mkuu wa shule aeleza uhalifu ulivyo shuleni

Muktasari:

  • Katika taarifa hii ya uchunguzi, jana tuliona jinsi wanafunzi wa shule tano za sekondari katika Jimbo la Ukonga mkoani Dar es Salaam wanavyojihusisha na vitendo vya uhalifu kama wizi, uporaji wa kutumia silaha, uvutaji dawa za kulevya, uchezaji kamari na unywaji pombe. Walimu na wanafunzi walioongea na mwandishi wetu walithibitisha kuwepo kwa vitendo hivyo. Leo pamoja na mambo mengine mwandishi anasimulia jinsi vikundi vinavyofanya kazi. Sasa endelea…

Dar es Salaam. Ni kawaida kwa mwanafunzi kuadhibiwa na walimu kwa makosa ya kinidhamu, lakini kwa Sekondari ya Charambe hali ni tofauti; wanafunzi 27 wamepelekwa kituo cha polisi cha Sitakishari wakihusishwa na uhalifu ndani ya miaka mitano.

Kati ya hao, mmoja alipelekwa kwa kosa la kumtishia mwanafunzi mwenzake kwa kisu wakiwa chooni, akimlazimisha atoe fedha.

“Hii shule ina wanafunzi hatari, lakini tunajitahidi kupambana nao,” anasema mwalimu mkuu shule hiyo, Paul Lorri.

“Wakati ninafika hapa mwaka 2013, katika darasa lenye wanafuzi 200 unakuta wanaohudhuria vipindi vyote ni wanne au saba. Wengine wote walikuwa wanaishia mitaani.”

Anasema nidhamu ya wanafunzi ilikuwa mbovu kiasi cha kushusha ufaulu na alikuta shule inafaulisha mwanafunzi mmoja au wawili, lakini sasa wamefikisha 70.

Kuhusu utovu wa nidhamu, Lorri anasema shule hiyo imewafikisha Sitakishari wanafunzi 27 ndani ya miaka mitano kwa matukio ya uhalifu.

Anasema miongoni mwa matukio hayo ni lile la mwanafunzi kutishia kumchoma kisu mwenzake wakati wakiwa chooni akimtaka atoe pesa. “Liliwahi kutokea tukio moja hapa la mwanafunzi kumtolea kisu mwanafunzi mwenzake chooni na kumtishia kumuua asipotoa pesa,” anasema Lorri.

Anasema baada ya kugoma kutoa fedha, mwanafunzi mwenye kisu alimchukua mwenzake kwa nguvu na kumpeleka kwenye kundi la wenzake. “Taarifa ilisambaa haraka. Nikamwambia makamu wangu afuatilie alikopelekwa yule mwanafunzi. Wakati anaondoka mimi pia nilitoka, nikapita njia nyingine.”

Anasema kabla makamu wake hajafika, alikutana na mwanafunzi huyo akiwa anarudi na kutishia kumpiga, lakini alimkabili na kumkamata kwenda kumhifadhi shuleni. “Baadaye tulimwachia, mwanafunzi huyo aliacha shule baada ya muda mfupi,” anasema mwalimu huyo.

“Niseme kwa sasa walau shule imetulia. Wamebaki wakorofi wachache, lakini tunapambana nao. Hapa shuleni tuna vijana wetu ambao tumewapa kazi ya kulinda usalama. Ni kama wapelelezi, wakipata taarifa zozote za mwenendo mbaya wa wanafunzi wanatoa taarifa haraka na tunazifanyia kazi.” Lorri anasema shule imekuwa ikialika taasisi mbalimbali kutoa elimu ya kujitambua na zinafanya kazi nzuri.

Makundi matatu

Uchunguzi wa Mwananchi, umebaini kuwapo kwa makundi ya aina takriban tatu ya wanafunzi wanaofanya uhalifu.

Wapo wanafunzi wanaounda vikundi ndani ya shule na kutekeleza uhalifu dhidi ya wenzao na wakati mwingine nje ya shule. “Hata hapa shuleni tuna kikundi cha aina hiyo, kazi yao ni kupora, kuiba, kupiga, kuuza na kuvuta bangi na kucheza kamari,” anasema mwalimu mkuu wa Sekondari ya Furaha, Simon Chumila.

Aina ya pili ni makundi yanayojumuisha wanafunzi kutoka shule tofauti za maeneo ya karibu, yaani kundi linaweza kuundwa na wanafuzi sita kutoka shule tatu. Kundi la tatu ni lile linaloundwa na mchanganyiko wa wanafunzi na vijana wengine wa mitaani ambao hupora na kuuza bangi.

Katika kabati lake, mwalimu Chumila ana jalada la kesi za wanafunzi ambao wamekuwa wasimamishwa shule kwa muda au kufukuzwa kutokana na utovu wa nidhamu.

Katika kile kinachoonekana kuwa mienendo ya wanafunzi imeathiri jamii, baadhi ya shule zimekuwa zikiomba uthibitisho kutoka kwa wakazi wa Serikali za mitaa unaoonyesha kuwa mwanafunzi aliyekuwa amesimamishwa amebadilika tabia.

Mwananchi limeona barua kutoka ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Mongolandenge, Kata ya Ukonga kwenda kwa mkuu wa Sekondari ya Furaha. Barua hiyo inaomba mwanafunzi mmoja (jina linahifadhiwa) apokewe shuleni baada ya kupewa adhabu ya kukaa nyumbani.

Barua nyingine ya Julai 16 ni ya mwanafunzi anayeomba radhi kwa uongozi wa shule baada ya kukutwa na panga katika begi.

Usikose mfululizo wa makala hizi ambapo katika toleo la kesho walimu wakuu wanaeleza jinsi wanavyokabiliana na tabia za wanafunzi na namna takwimu za Jeshi la Polisi kwa kiasi kikubwa zinavyothibitisha tatizo.