Mloganzila yagawa bure miwani kwa wagonjwa wa macho

Wagonjwa mbalimbali wakipimwa ugonjwa wa  kisukari katika maadhimisho ya Wiki ya Kisukari Hospitali ya Taifa Muhimbili tawi la Mloganzila,

Muktasari:

  • Ugonjwa wa kisukari au shinikizo la damu unaweza usiwe na dalili za kumfanya mtu atafute tiba hadi pale macho, figo, moyo au mishipa ya damu au fahamu inapokuwa imeharibika vibaya kabla ya kusababisha dalili.

Dar es Salaam. Katika maadhimisho ya Wiki ya Kisukari Hospitali ya Taifa Muhimbili tawi la Mloganzila, linapima magonjwa mbalimbali yanayoambatana na kisukari ikiwemo ugonjwa wa macho na kugawa miwani bure.

Tangu Novemba 12 zaidi ya watu 760 wamejitokeza kupima magonjwa mbalimbali ikiwemo kisukari na macho.

Akizungumza leo Novemba 14 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kisukari Duniani yanayofanyika katika tawi la Mloganzila, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Profesa Lawrence Museru amesema wanatoa miwani bure kwa wote wanaobainika kuwa na matatizo.

Profesa Museru amesema katika kuitikia wito wa kuadhimisha Siku ya Kisukari Duniani, MNH tawi la Mloganzila wanatoa bure huduma za uchunguzi wa afya kwa wananchi wote kwa siku tano hadi Novemba 16.

“Tunawakaribisha wananchi kufika katika Hospitali ya Mloganzila kuendelea kuja hadi Novemba 16 ili kupimwa afya zenu, tunapima kisukari, shinikizo la damu, uchunguzi wa macho na utoaji wa miwani kwa watakaobainika kuwa na tatizo, uchunguzi wa afya ya kinywa na meno pamoja na upimaji na elimu kuhusu lishe bora,” amesema.

Profesa Museru amesema katika kutoa huduma hizo bure wadau mbalimbali wameshiriki ikiwemo Bohari ya Dawa (MSD) ambao wametoa vifaa vya kupimia na wadau ambao wameshirikiana nao katika kuandaa Wiki ya Kisukari na kuwezesha kwa namna mbalimbali utoaji wa huduma za upimaji.