Mmiliki kampuni ya mabasi ya Muro akwepa kifungo, alipa faini

Muktasari:

Mmiliki wa Kampuni ya mabasi ya Muro, Majid Kimaro amekwepa kifungo cha miaka nane jela kwa kulipa faini ya Sh115milioni baada ya kutiwa hatiani na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.


Dar es Salaam. Mmiliki wa Kampuni ya mabasi ya Muro, Majid Kimaro amekwepa kifungo cha miaka nane jela kwa kulipa faini ya Sh115milioni baada ya kutiwa hatiani na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Leo Jumatano Desemba 12, 2018 Muro amehukumiwa  kulipa faini ya Sh115milioni au kutumikia kifungo cha miaka nane jela.

Muro alikiri shtaka la kutakatisha fedha na kuongoza genge la uhalifu ili kuiba mafuta katika bomba linalomilikiwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).

Anakabiliwa na  mashtaka mawili likiwemo la kuongoza genge la uhalifu katika  kesi  ya uhujumu uchumi namba 81/2018 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Katika hukumu hiyo pia mahakama hiyo imeamuru gari aina ya Scania lenye namba za usajili T 856 ADH ambalo lilitumika kuiba mafuta zaidi ya lita 26,875.25 ya dizeli na petroli  litaifishwe na kuwa mali ya Serikali.

Akitoa hukumu hiyo Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba amesema kuwa mahakama inamtia hatiani mshtakiwa kwa makosa mawili baada ya kukiri.

Simba amesema katika shtaka la kwanza la kuongoza genge la uhalifu, Muro anapaswa kulipa faini ya Sh5milioni au kifungo cha miaka mitatu jela.

Katika shtaka la utakatishaji fedha mshtakiwa atatakiwa kulipa faini ya Sh110milioni  au kifungo cha miaka mitano jela.

Kabla ya kutolewa adhabu hiyo, wakili wa Serikali Simon Wankyo akisaidiana na Jacqueline Nyantori na Patrick Mwita wameiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa washtakiwa kwa sababu makosa hayo ya wizi husababisha kuathirika kwa uchumi na nchi kukosa mapato.

Pia ameomba gari hilo litaifishwe na kuwa mali ya Serikali kwa sababu ndio lililotumika kubeba mafuta baada ya kulitoboa bomba  na kuiba mafuta hayo.

Wankyo amedai katika kesi ya msingi, mshtakiwa anadaiwa kati ya Julai Mosi, 2016 na Januari 8, 2018 katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Kigamboni, Dar es Salaam na maeneo mengine akiwa pamoja na wenzake ambao hawako mahakamani,  kwa kujua aliongoza genge la uhalifu kwa lengo la  kutoboa bomba la mafuta la TPA na kuiba mafuta ili kupata faida.

Katika shtaka la pili inadiawa kati ya Julai Mosi, 2016 na Januari 8, 2018 walipata lita 15,950.3  za mafuta ya dizeli na lita 10,925.22 za petroli na kusambaza mafuta hayo kwenye vituo vyake vya mafuta ma kuyauza wakati akijua yametokana na makosa ya uhalifu.