Mnenguaji Aisha Madinda afariki dunia

Muktasari:

Taarifa zilizotufikia kutoka kwa watu wa karibu wa Aisha zinasema kuwa mnenguaji huyo alifika hospitalini hapo kwa ajili ya matibabu na mauti kumkuta hapo hapo hospitalini huku sababu za kifo chake zikiwa bado hazijafahamika.

Dar es Salaam. Aliyekuwa mnenguaji mahiri wa bendi ya Twanga Pepeta na Extra Bongo, Aisha Madinda amefariki dunia leo katika Hospitali ya Mwananyamala, jiji Dar es Salaam.

Taarifa zilizotufikia kutoka kwa watu wa karibu wa Aisha zinasema kuwa mnenguaji huyo alifika hospitalini hapo kwa ajili ya matibabu na mauti kumkuta hapo hapo hospitalini huku sababu za kifo chake zikiwa bado hazijafahamika.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mwananyamala, Dk. Sophinias Ngonyani alithibitisha kifo hicho na kuongeza kuwa wauguzi waliuona mwili wa marehemu ukiwa hospitalini hapo na kutoa taarifa ambapo ulichukuliwa na kuhifadhiwa kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi.

 “Hatujafahamu amekufa kwa ugonjwa gani kwasababu hadi mauti yanamkuta alikuwa bado hajapokelewa na kupatiwa huduma, Aisha pamoja na huyo rafiki yake wamekuwa wakihudhuria hospitalini hapa mara kwa mara kwa ajili ya matibabu maalum,” alisema Dk Ngonyani.

Aisha anatajwa kuwa miongoni mwa wasanii wanaopata matibabu ya kuondoa Uraibu wa matumizi ya dawa za kulevya.