Mnyeti awashitaki maofisa wa Wizara ya Elimu kwa Makamu wa Rais

Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti akizungumza Wilayani Hanang. Picha na Joseph Lyimo

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti amemweleza Makamu wa Rais, Samia Suluhu kuwa baadhi ya maofisa wa Wizara ya Elimu, wanafuja fedha za ujenzi wa madarasa na mabweni ya Shule ya Sekondari ya Wasichana Nangwa. Amesema mkoa wake si wa majaribio ya ufisadi.

Hanang'. Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti amemweleza Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan kuwa baadhi ya maofisa wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, wanafuja fedha za ujenzi wa madarasa na mabweni ya Shule ya Sekondari ya Wasichana Nangwa.

Mnyeti ameyasema hayo leo Jumapili Novemba 18, 2018 wakati akimkaribisha Makamu wa Rais Samia, kuweka jiwe la msingi mabweni ya Shule ya Sekondari ya Wasichana Nangwa iliyopo wilayani humo.

Amesema maofisa hao wa Wizara ya Elimu wametumia zaidi ya Sh807 milioni kujenga madarasa na mabweni wakati bweni lingine kubwa zaidi limejengwa na halmashauri kwa Sh150 milioni.

"Mheshimiwa Makamu wa Rais nataka nikuhakikishie mkoa huu si wa majaribio wa watu kufuja fedha kwani nikiwaandikia barua wanipe taarifa wanadai jengo linajengwa na wizara si mkoa," amesema Mnyeti.

Amesema Makamu wa Rais na Rais John Magufuli wanatumia nguvu kubwa kutafuta fedha za kujenga miundombinu ya shule lakini baadhi ya watu wanafuja fedha hizo.

"Nimeshaagiza uchunguzi ufanyike kwani wanapaka rangi majengo na kukarabati mengine kwa kutumia gharama kubwa bila sababu," amesema Mnyeti.