Mnyukano wa korosho wazidi kupamba moto

Muktasari:

Wakati Serikali ikiwataka wanunuzi watoe maelezo ya lini watanunua na kiasi gani, wadau wametoa kauli nzito, mbunge mmoja ametia neno uzito

Dar es Salaam. Huku Serikali ikitoa siku nne kwa kila kampuni iliyosajiliwa kuandika barua ya kuainisha itanunua tani ngapi za korosho, baadhi ya wanunuzi hao wamesema kuna ugumu wa utekelezaji wa agizo.

Wanunuzi hao wanadai uamuzi wa kununua korosho kwa kiwango gani haufanywi nchini.

Jana, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema ofisi yake itakuwa wazi kwa saa 24 kuzipatia nafasi kampuni 35 kueleza mipango ya kununua zao hilo.

Wakati Serikali ikitoa masharti hayo, baadhi ya wanunuzi wa korosho waliozungumza na Mwananchi walisema kuna ugumu wa utekelezaji wa agizo hilo kwa sababu wawakilishi wa kampuni waliopo nchini si wale wanaotoa uamuzi wa mwisho.

Wanunuzi, wachumi

Mwakilishi wa kampuni ya OM Agro, Zawadi Mohammed alisema, “Tumepeleka taarifa kwa mabosi India, wamesema wanahitaji kulifanyia kazi agizo hilo. Kwanza awasiliane na wateja wake. Lakini, si lazima kununua korosho, anaweza kuamua kuhamia kwenye zao jingine.”

Mwakilishi huyo alisema kinachofanyika ni bosi wake kuagiza kiasi gani kinunuliwe na inapobidi kuongeza, hivyo hawezi kuwa na uhakika ni kiwango gani anaweza kukiandika na kukipeleka kwa Waziri Mkuu kama alivyoagiza, bali ni hadi atakapoelezwa na mnunuzi mkuu.

Mchumi na mhadhiri mwandamizi wa Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDBS), Dk Mutahyoba Baisi alisema kwa kuwa Serikali imeshatoa msimamo wake hadharani, ni lazima korosho zitanunuliwa.

Msomi huyo alisema kwa ahadi ambazo Serikali imekuwa ikizitoa hakuna namna nyingine ya kuifanya iaminike katika suala hilo zaidi ya kuhakikisha inazitimiza ahadi hizo.

Mwanzo wa tatizo

Mwenendo usioridhisha wa uuzaji wa korosho nchini ulidhihirika zaidi baada ya mnada uliofanyika wilayani Newala na Tandahimba mkoani Mtwara kuvunjika kutokana na wakulima kugoma kuuza kilo moja kwa Sh2,717 iliyokuwa bei ya juu wakati Sh1,711 ikiwa ya chini.

Kadhia hiyo ilitokea Oktoba 22, kwenye mnada uliofanyika Kijiji cha Makukwe kilichopo Wilaya ya Newala mbele ya Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba licha ya kuhudhuriwa na kampuni 15.

Katika mnada wa kwanza mwaka jana, kilo moja ilinunuliwa kwa Sh3,850 na msimu huu wakulima walitarajia kupata bei nzuri zaidi.

Mgomo wa wakulima hao uliungwa mkono na Rais John Magufuli ambaye aliagiza kurudishwa wizarani kwa aliyekuwa kaimu mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Profesa Wakuru Magigi kwa madai kuwa ameshindwa kusimamia ununuzi wa zao hilo.

Kuhamishwa kwa mkurugenzi huyo kulienda sambamba na kusimamishwa kwa minada ya zao hilo kuanzia Oktoba 26 hadi iliporuhusiwa kuanzia Novemba Mosi.

Wiki moja mbele baada ya wanunuzi kufanya kama walichofanya wakulima, akiwa ofisini kwake jijini Dodoma, Majaliwa alitoa msimamo wa Serikali kwa wanunuzi hao walioelekezwa na Rais Magufuli kununua kilo moja kwa bei isiyopungua Sh3,000 kwa kilo.

Kwa mara ya pili ndani ya wiki mbili, Serikali imelazimika kusitisha tena minada ya korosho katika mikoa ya Lindi na Mtwara ingawa bado wakulima nchini hawajui hatima yao kutokana na bei kutetereka. Minada hiyo imesitishwa baada ya wanunuzi kutojitokeza.

Wadau wa korosho

Akichangia mapendekezo ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka 2019/20 bungeni jana, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CCM), Peter Serukamba aliiomba Serikali kuacha nguvu ya soko iamue bei ya bidhaa.

Alisema kilimo - biashara ndicho kitakachomaliza changamoto zilizopo.

“Matatizo ya kilimo yatatatuliwa na uwepo wa mashamba makubwa, Mungu katupa ardhi na watu wenye uwezo mkubwa watakuja,” alisema.

Mkulima wa korosho wilayani Tunduru, Mukatesi Majura alisema hana wasiwasi na anaamini atauza mzigo alionao ingawa si kwa wakati aliopanga.

“Serikali huwa inanunua mahindi. Imenunua Bombardier na inajenga reli ya kisasa itashindwaje korosho? Rais alishasema, soko la China litakuwa vizuri kuanzia Desemba, tunasubiri,” alisema Mukatesi.