Mo Salah awaliza mashabiki wa Napoli

Muktasari:

Mshambuliaji nyota wa Misri Mohamed Salah, jana alifunga bao muhimu kwenye Uwanaj wa Anfield lililoihakikishia Liverpool ushindi wa 1-0 dhidi ya Napoli ya Italia na kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kutoka kundi C ikiungana na PSG ya Ufaransa, huku Napoli ikiangukia kwenye Europa Ligi


Liverpool, England. Bao la mshambuliaji nyota kutoka Misri, Mohamed Salah, katika mchezo wa mwisho wakundi C uliochezwa jana usiku kwenye Uwanja wa Anfield liliwatoa machozi mashabiki wa Napoli.

Hata hivyo kilichoiingiza Liverpool katika hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, wakiipiku Napoli sio bao la Salah, bali ni bao walilofunga katika mechi ya ugenini dhidi ya Napoli walipofungwa 2-1.

Salah alifunga bao hilo katika dakika ya 34 akiwatoka wachezaji wawili wa Napoli na kufyatua kombora lilija pembeni mwa goli na kumshinda kipa David Ospina, hivyo Liverpool kufikisha pointi tisa sawa na Napoli.

Kosa la kucheza kwa kujihami lilikaribia kumharibia kocha Jurgen Klopp kwani walikaribisha mashambulizi mengi na kama washambuliaji wa Napoli wangekuwa makini wangepata mabao.

Aisha Liverpool wanapaswa kumshukuru kipa Alisson Beckerambaye alifanya kazi ya ziada kupangua mashuti mengi yaliyoelekezwa langoni mwake, nafasi ambayo Napoli wataijutia zaidi ni ile ya Arkadiusz Milik ambaye alipiga kwa pupa na kipa huyo kuokoa.

Liverpool ambayo kwa mara ya kwanza msimu huu ilipoteza mechi zote za ugenini za mashindano hayo na kushinda zote za nyumbani, wamefikisha pointi tisa na kuishusha Napoli ambayo ilikuwa ikiongoza kundi C ambapo ushindi wa PSG wa mabao 4-1 dhidi ya Red Stars umeipeleka kileleni ikifikisha pointi 11.

Kwa matokeo hayo Napoli sasa inaagukia kwenye michuano ya Europa Ligi, na kuziacha Liverpool na PSG zikitinga katika hatua ya 16 bora ya michuano hiyo.

Kocha Jurgen Klopp alimwagia sifa Salah kwa kufunga bao hilo, ikiwa ni siku tatu tangu alipoifunjgia mabao matatu ‘hat trick’ Liverpool ikiizamisha Bournemouth kwa mabao 4-0 katika mechi ya Ligi Kuu England na kukaa kileleni mwa Ligi hiyo.

Alisema nyota huyo ambaye msimu uliopita alikuwa mfungaji bora wa timu hiyo na Ligi Kuu England kwa ujumla wake kwa sasa amerejea kwenye kiwango chake bora.

Matokeo ya jumla ya Ligi ya Mabingwa Ulaya hapo jana: Schalke 1 Lokomotiv Moscow 0, Galatasaray 2 FC Porto 3, Club Brugge 0 Atl Madrid 0, Monaco 0, B Dortmund 2, Barcelona 1 Tottenham 1, Inter Milan 1 PSV Eindhoven 1, Red Star Belgrade 1 PSG 4 na    Liverpool 1 Napoli 0.

Kutokana na matokeo hayo timu zilizofuzu hadi sasa ya kwanza ikiwa kinara wa kundi ni Kundi A, B. Dortmund, Atletico Madrid, kundi B, Barcelona na Tottenham Kundi C,  PSG na Liverpool, Kundi D, FC Porto na Schalke.

Kundi E, Bayern Munich na Ajax, kundi F Manchester City wakati mechi za leo usiku zitaamua hatima ya Lyon na Shakhtar, Kundi G, Real Madrdi na AS Roma, wakati Kundi H ni Juventus na Manchester United