Mpagazi jela maisha kwa kulawiti watoto watatu

Moshi. Kijana aliyekuwa anajihusisha na kazi ya kuwapandisha watalii katika Mlima Kilimanjaro, George Lesilwa amehukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kulawiti watoto watatu wa kiume.

Mtuhimiwa huyo sasa amehukumiwa kifungo cha maisha kwa kila kosa katika makosa hayo matatu.

Lesilwa, mkazi wa Mnazi Kiborlon mjini Moshi alipatikana na hatia ya kuwalawiti watoto hao ambao ni wa wapangaji wenzake kwa kuwapa Sh500 kwa kila tendo.

Kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa mahakamani, udhalimu huo ulibainika baada ya mmoja wa wazazi kukuta Sh500 kwenye daftari la mtoto wake na alipomhoji alikoitoa ndipo alipomtaja Lesilwa.

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, Pamela Mazengo baada ya kuridhishwa na ushahidi wa mashahidi saba wa upande wa mashtaka.

Hakimu Mazengo alisema ushahidi wa mashahidi hao waliotoa ushahidi wao kwa kuongozwa na mawakili wa Serikali,Ignas Mwinuka na Grace Kabu haukuacha mashaka kuwa mtuhumiwa alitenda makosa hayo. Awali, mawakili hao walidai kuwa katika siku na saa zisizojukana Oktoba 2017, mshtakiwa aliwaingilia kinyume cha maumbile watoto hao watatu wenye umri wa kati ya miaka 7 na 9.

Katika utetezi wake, mshtakiwa alikanusha akidai amefunguliwa mashtaka hayo kutokana na kile alichodai ni visa vya baba mwenye nyumba aliyokuwa akiishi na wazazi wa watoto hao.

Hata hivyo, Hakimu Mazengo alisema utetezi huo hauna mashiko kwa vile mwenye nyumba hana mtoto aliyefanyiwa vitendo hivyo.

Alisema hata katika ushahidi wa msingi walioutoa wapangaji dhidi yake, ilidhihirika kuwa hawakuwa na chuki nao na mshtakiwa alikiri hilo alipoulizwa maswali kortini.

Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, mawakili waliokuwa wakiendesha kesi hiyo waliiomba mahakama itoe adhabu kali kwa mujibu wa sheria ikizingatiwa kuwa watoto waliofanyiwa kitendo hicho ni wa chini ya miaka 12.

Akisoma hukumu, hakimu huyo alisema mahakama hiyo imemtia hatiani mshtakiwa huyo na kwa kila shtaka la ulawiti aliloshtakiwa nalo atatumikia kifungo cha maisha jela ili iwe fundisho kwa wanaodhamiria kufanya tendo kama hilo.

Hakimu Mazengo alisema matukio ya watoto kudhalilishwa kwa kubakwa na kulawitiwa yanashika kasi kutokana na mmomonyoko wa maadili katika jamii, hivyo njia pekee ya kupambana na hali hiyo ni adhabu kali kwa wahusika.