Msekwa amkosoa Dk Bashiru kuhusu Membe

Muktasari:

  • Baada ya Mvutano na majibizano kati ya Katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally na Mwanachama wa CCM  Bernard Membe,hatimaye aliyekuwa makamu mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa,ameibuka na Kuzungumzia sakata hilo.

Dar es Salaam. Katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally alimwambia Bernard Membe kuwa kumpa sharti la kukutana naye si utaratibu wa chama hicho, lakini mtendaji huyo mkuu wa CCM naye ameelekezwa utaratibu unaotakiwa.

Na maelekezo hayo yanatoka kwa aliyekuwa makamu mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa, ambaye pia ameshangazwa na kitendo cha kutumia jukwaa kuita wanachama ofisini.

Msekwa alisema hayo wakati alipoulizwa na Mwananchi kuhusu malumbano baina ya Dk Bashiru na mtu anayeitwa Bernard Membe ambaye alijitokeza kwenye mitandao ya kijamii kujibu tuhuma kwamba anataka kumkwamisha Rais John Magufuli kurudi Ikulu mwaka 2020.

Membe hajajitokeza kuthibitisha kama akaunti iliyomjibu Dk Bashiru ni yake.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Dk Bashiru aliwaambia wanachama wa CCM kuwa wanahitaji umoja hata kama baadhi walishindwa katika uchaguzi.

Alisema hata waliotaka kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho wameonyesha mshikamano na ameshazungumza nao isipokuwa Membe tu, na akamtaka afike ofisini kwake kujibu tuhuma kuwa anataka kumuhujumu Magufuli.

Hata hivyo, akaunti hiyo ilimjibu Dk Bashiru kuwa Membe yuko tayari kukutana naye, lakini ikataka na mtu anayetoa tuhuma hizo awepo siku hiyo ili athibitishe tuhuma zake, kitu ambacho katibu huyo wa CCM alisema si utaratibu wa chama kuweka sharti.

Hata hivyo Msekwa aliliambia Mwananchi jana kuwa njia aliyotumia Dk Bashiru iko nje ya utaratibu wa CCM pale kinapohitaji kushughulikia tuhuma dhidi ya mwanachama wake.

Msekwa alisema alichotakiwa kukifanya ni ama kumpigia simu Membe au kumwandikia barua ambayo ingemtaka afike ofisini kwake, badala ya kutumia jukwaa la mkutano wa hadhara.

“Hii approach (njia) sijaipenda,” alisema Msekwa, ambaye pia aliwahi kuwa spika wa Bunge la Jamhuri kwa vipindi viwili.

“Mimi nimewahi kuwa katibu mkuu mtendaji wa chama, sikufanya hivyo na hata kama ningekuwa sasa, kama nahitaji kuonana na kiongozi au mwanachama fulani nilikuwa ninamuita moja kwa moja kwa simu ofisini kwangu.

“Kutangaza hadharani haina maana yoyote. Kuna taratibu za kazi, sasa kukiuka siyo jambo jema hata kidogo, hilo sikulipenda.”

Alisema kama Membe angekuwepo katika mkutano huo, angeweza kumuagiza waonane baadaye.

“Lakini wewe uko mkoa mwingine yeye yuko mkoa mwingine, halafu wewe unaagiza tu aje, je asiposikia tangazo lako? Unajuaje alikuwa anasikiliza wakati huo? Je, asipokuja utamlaumu? Kuna utaratibu wa kazi, anapigiwa simu ama anaandikiwa barua.”

Membe alikuwa mmoja wa wanachama 38 wa CCM waliochukua fomu kutaka kugombea urais kwa tiketi ya CCM mwaka 2015, lakini aliishia tano bora alipoenguliwa na Halmashauri Kuu.

Tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu amekuwa hajishughulishi na siasa zaidi ya kuonekana katika shughuli za kijamii.

‘Anamkwamishaje Magufuli?’

CCM ina utamaduni wa kumuachia mwanachama aliyeshinda uchaguzi wa Rais apitishwe kugombea urais bila ya ushindani ndani ya chama na kauli ya Dk Bashiru inaonekana kutaka kuendeleza utamaduni huo.

Hata hivyo, Mwananchi ilipomuuliza katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (siasa, uhusiano na kimataifa), Kanali Ngemela Lubinga kama kauli hiyo ya Dk Bashiru inaweza kujenga hofu wanachama na kujizuia kuchukua fomu za urais mwaka 2020, alijibu haitawazuia kwa kuwa katiba ya chama hicho ya 2012 na mabadiliko ya 2017 yameweka wazi suala hilo.

“Wanachama wanaruhusu kugombea, lakini si utamaduni (wetu) mpaka miaka kumi iishe,” alisema Lubinga.

“Lakini hakuna kizuizi, Katiba inasema kila miaka mitano tutafanya uchaguzi. Tafuta katiba ya 2017 hata ile ya 2012, inaeleza yote.”

Kanali huyo mstaafu alisema hakuna mwiko wa kugombea nafasi hiyo kubwa ya kisiasa kushindana na rais aliyeko madarakani, bali akasema cha muhimu ni kuzingatia muda wa kutangaza hiyo nia.

“Kwani kugombea ni mwiko? Usisahau 2015 kulikuwa na zaidi ya wagombea 40,” alisema Lubinga.

“Kugombea si tatizo, kutangaza nia mapema ni kosa. Kuna wakati wa kutangaza nia, siyo muda wowote.

“(Kitendo cha kutangaza nia) Kitamkwamishaje (Magufuli)? Haimkwamishi chochote, isipokuwa tumeweka utaratibu kwamba kuna wakati wa kampeni. Mimi ndiyo niliandika utaratibu huo kwamba ni kosa kwa mujibu wa kanuni zetu.”

Dk Bashiru na Membe

Mwaka 2014, Membe alikuwa mmoja wa wanachama sita wa CCM waliofungiwa kwa miezi 12 kujihusisha na siasa kwa madai ya kuanza kampeni za urais mapema. Wengine ni Edward Lowassa na Frederick Sumaye, ambao baadaye walihamia Chadema, William Ngeleja, January Makamba na Stephen Wasira.

Na Dk Bashiru anakariri taarifa zinazomtuhumu Membe kuwa anafanya vikao ya kutafuta urais kabla ya muda na ndio maana anataka aende ofisini kwake kujibu tuhuma.

“Iweje watu waseme kwamba wewe (Membe) unafanya vikao vya kutafuta kura za 2020..kwamba unataka kumkomesha Rais Magufuli, halafu unakaa kimya tu? Sasa mimi nakualika uje ofisini kama ni mwanachama wa kweli aliyetoa ahadi ya uanachama wa CCM.”

Hata hivyo, jana jioni CCM ilitoa msimamo wake kuhusu hatua hiyo ya Dk Bashiru kwa Membe.

Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole ilisema kauli ya Bashiru kumtaka Membe kufika ofisini kwake ni ya kawaida ndani ya CCM.

“Ni utaratibu wa kawaida wa katibu mkuu kukutana na viongozi na wanachama wa CCM kuimarisha umoja na mshikamano,” alisema.

“CCM inapenda kuwafahamisha kuwa imefuatilia kwa ukaribu mjadala unaoendelea kwenye mitandao ya kijamii kuhusu wito alioutoa Bashiru kwa Membe,” inaeleza taarifa hiyo.

“Ni kama sehemu ya utaratibu wa kawaida wa Katibu Mkuu kukutana na viongozi na wanachama wa CCM katika kuendelea kuimarisha umoja na mshikamano wa wanachama.”

Chama hicho kimetoa rai kwa Watanzania kuwa wito huo ulikuwa ni wa kawaida hivyo uzushi, uchonganishi, fitina na uvumi mwingine wowote unaoendelea katika mitandao ya kijamii ina hila mbaya kwa CCM.