Msekwa awajibu wanaohoji uteuzi wake kuwa mkuu wa MUST

Muktasari:

Spika wa  Bunge Mstaafu, Pius Msekwa amesema ana uzoefu mkubwa wa kuongoza vyuo vikuu nchini Tanzania na kuahidi kuleta mabadiliko makubwa katika chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia (MUST)

Mbeya. Spika wa  Bunge Mstaafu, Pius Msekwa amesema uteuzi wake wa kuwa mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia (MUST) uliofanywa na Rais John Magufuli Desemba 6 ,2018 hakukosea na kwamba anatambua utendaji wake na uzoefu alionao kwa kuongoza baadhi ya vyuo vikuu nchini Tanzania kikiwapo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm).

Alisema hayo leo Jumamosi Desemba 15, 2018 alipokuwa akizungumza katika mahafali ya sita ya chuo hicho, ambapo alikuwa kivutio kutokana na staili yake ya kutumia vifungu vya biblia na kutoa mifano ya namna alivyokuwa akiliendesha Bunge.

"Kwanza kuna kila sababu ya kumshukuru Rais kwa kuniona mimi nafaa kuvaa kiatu hiki kwani kuna watu wengi serikalini lakini kaona mimi ndiye sahihi zaidi, nitaitumia fursa hii kuboresha elimu ya sayansi na teknolojia sambamba na kuongeza udahili kwa mwaka 2019/2020," alisema.

Msekwa alisema kupitia nafasi hiyo atahakikisha chuo hicho kinakuwa chachu ya kuzalisha wataalamu wa nyanja mbalimbali na kwamba amekuwa na bahati ya kuteuliwa kwa awamu ya tatu sasa kuongoza vyuo vikuu nchini.

Naye mwenyekiti wa baraza la chuo hicho, Zakia Meghji alishauri uongozi wa chuo hicho kufanya tafiti katika nyanja mbalimba ili kuchochea maendeleo ya uchumi wa viwanda.

Alisema mafanikio ya chuo hicho yanatokana na jitihada za Serikali kutatua changamoto zinapojitokeza.

Makamu mkuu wa chuo hicho, Profesa Joseph Msambichaka alisema wana mikakati ya kuanzisha mfuko kwa ajili ya kusomesha wanafunzi wa  kike sambamba na kujenga maabara ya kisasa itakayochukua wanafunzi 2,000 kwa wakati mmoja.

Alisema wameanza kutoa mafunzo ya uhandisi wa vifaa tiba kwa ajili ya kuwezesha hospitali za mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kuboresha huduma za afya na kufanyiwa matengenezo vifaa hivyo ili kuipunguzia Serikali gharama kubwa inayotumia kutumia wataalamu wa  nje ya nchi.