Msomi akosoa maneno katika pasipoti mpya

Muktasari:

Ni aliyekuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Joseph Mbele. Amesema maneno yaliyomnukuu mwalimu Julius Nyerere yamekosewa.


Dar es Salaam. Aliyekuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Joseph Mbele amedai hati mpya za kusafiria zimekosewa baadhi ya maneno yanayomnukuu mwalimu Julius Nyerere.

Msomi huyo ameibua jambo hilo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa  Facebook na kuzua mjadala mzito miongoni mwa jamii.

Maneno hayo yameandikwa kwa Kiingereza na tafsiri  yake inasomeka “Sisi tumekwisha uwasha Mwenge wa uhuru na tumeuweka juu ya Mlima Kilimanjaro. Umulike ndani na nje ya mipaka yetu, ulete tumaini pale ambapo hakuna matumaini, ulete upendo mahali penye chuki na heshima palipojaa dharau,” Mwl Julius K. Nyerere (09/12/1961). Kosa linaloonekana ni kushindwa kutofautisha nyakati kati ya ‘tumeweka’ badala ya ’tuliuweka’.

Profesa Mbele amesema makosa hayo ni aibu kwa Taifa huku akisema ipo haja ya kurudia kutengeneza pasipoti hizo.

“Nimethibitisha makosa yaliyopo kwenye ukurasa wa 47, ni jambo la kuudhi. Kiufupi Pasipoti hizi mpya zinatakiwa kutengenezwa upya hata kama itagharimu kiasi kikubwa cha fedha,” amesema msomi huyo.

Alipoulizwa kuhusu jambo hilo Ofisa Mawasiliano wa Idara ya Uhamiaji, Ally Mtanda amesema bado hawana taarifa juu ya suala hilo.

“Bado hatujakutana na malalamiko kama hayo, tafadhali nitumie ili niweze kuwasilisha kwa mabosi kabla ya kuizungumzia baadaye,” amesema.

Alipotafutwa tena amesema amewasilisha suala hilo kwenye uongozi lakini hakuweza kulitolea ufafanuzi.