Makongoro Nyerere afunguka urais

Friday March 6 2015Makongoro Nyerere

Makongoro Nyerere 

By Florence Majani, Mwananchi

Dar es Salaam. Wakati CCM ikielekea katika kipindi kigumu cha kuamua mgombea wake wa urais kwenye Uchaguzi Mkuu ujao, Makongoro Nyerere, ambaye ni mtoto wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, amezungumzia taarifa zilizoenea kwenye mitandao ya kijamii zikimtaja kuwa na mpango wa kuwania nafasi hiyo ya juu nchini.

CCM, ambayo imeshika nchi tangu kurejeshwa kwa siasa za vyama vingi, hujikuta katika wakati mgumu kila wakati inapotakiwa kutoa mgombea wa kurithi nafasi ya Rais aliye madarakani baada ya kuongoza vipindi viwili vya miaka mitano kila kimoja.

Tayari wanachama wanne wa chama hicho tawala wameshatangaza rasmi kuwania urais huku wengine sita wakifungiwa kwa makosa ya kudaiwa kuanza kampeni mapema, huku kukiwa na mlolongo wa watu wanaotajwa kuwa na mpango wa kujitokeza kuwania nafasi hiyo, akiwamo Makongoro, ambaye imeelezwa kuwa ameshauriwa kuchukua uamuzi huo kujaribu kukinusuru chama kutokana na makundi yanayoonekana kujitokeza katika mbio hizo.

“Mimi si mtabiri, siwezi kukwambia nitagombea au la, lakini uamuzi wangu utajulikana mara kipenga kitakapopulizwa na CCM,” alisema Makongoro ambaye ni ofisa wa zamani wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) na mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala).

Vyanzo hivyo vya habari vimeeleza kuwa mkakati wa kuhakikisha Makongoro anakuwa rais, unaratibiwa na baadhi ya makada waliowahi kufanya kazi na Mwalimu Nyerere.

Mkakati huo pia unatajwa kuwa ulianza pale alipochaguliwa kuwa mbunge wa Eala. Tayari Waziri Mkuu Mizengo Pinda, January Makamba, ambaye ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Lazaro Nyalandu ambaye ni Waziri wa Maliasili na Utalii na Hamisi Kigwangala (mbunge) wametangaza nia ya kuomba ridhaa ya CCM kuwapitisha kuwania urais.

Hata hivyo, upinzani mkubwa unaonekana kuwa kwa vigogo ambao hawajatangaza nia hiyo na ambao wanatumikia adhabu ya kufungiwa kwa zaidi ya miezi 12 kutokana na kikiuka taratibu za chama hicho.

Miongoni mwa ambao hawajajitokeza ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ambaye wafuasi wake wamekuwa wakijitokeza katika siku za karibuni kueleza wazi msimamo wao kuwa ndio chaguo sahihi, na Bernard Membe, ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Pia yumo Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye, Spika wa zamani wa Bunge, Samuel Sitta, Waziri wa Kilimo na Chakula, Steven Wasira na Naibu Waziri wa Fedha-Sera, Mwigulu Nchemba, ambaye alionywa na chama hicho dhidi ya safari zake mikoani zilizodaiwa kuwa na dalili za kampeni.

Kauli ya Makongoro

Akizungumza na gazeti hili, Makongoro hakuonyesha kukataa wala kukubali kuhusu uamuzi wa kugombea nafasi hiyo iliyoshikwa na baba yake kwa takribani miaka 25.

“Ninachoweza kutabiri kwa sasa ni iwapo nina njaa basi lazima nitakula au simba akitokea lazima nikimbie. Kama nina usingizi na kuna kitanda karibu lazima nitalala lakini mambo mengine siwezi kuyasemea,” alisema Makongoro ambaye aliwahi kuwa mbunge wa Arusha Mjini kwa tiketi ya chama cha NCCR-Mageuzi. Alisema anasubiri siku ambayo CCM itatangaza mchakato wa kuchukua fomu ndipo hatma yake itajulikana.

Makongoro ni nani

Makongoro ni mtoto wa tatu wa familia ya Hayati Nyerere na Januari 30 mwaka huu alitimiza miaka 56 tangu azaliwe. Alipata mafunzo ya uongozi wa kijeshi Monduli kati ya mwaka 1980 na 1982.

Luteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi alipata elimu ya sekondari ya juu na ya kawaida kwenye Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Tabora wakati elimu ya msingi alisomea katika shule tatu tofauti za Arusha, Bunge na Isike kati ya mwaka 1971 na 1978.

Mwaka 1995 Makongoro alihama CCM na kujiunga na NCCR Mageuzi na katika uchaguzi wa kwanza tangu kurejeshwa kwa siasa za vyama vingi, Makongoro alishinda ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini, lakini hakumaliza kipindi chake kutokana na ubunge huo kupingwa mahakamani na hatimaye kutenguliwa.

Aprili 7, 2012 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilimchagua kuingia kwenye Bunge la Afrika Mashariki.

Maoni ya wachambuzi

Alipoulizwa kuhusu taarifa hizo, mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku alisema masuala ya urais wa Makongoro aulizwe mwenyewe.

“Sitaki kuulizwa kuhusu hilo, mimi si meneja wa kampeni wa hao watu. Nitoe kabisa katika hilo,” alisema Butiku, ambaye ni miongoni mwa watu waliofanya kazi na Mwalimu Nyerere wakati wa utawala wa awamu ya Kwanza.

Mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale-Mwiru alisema hawezi kutoa maoni yoyote hadi pale Makongoro atakapoamua kutangaza nia ya kuwania nafasi hiyo.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana alisema iwapo Makongoro anahitaji kuwa rais, basi angepata kwanza ushauri wa wazee kutoka Butiama.

“Kwangu mimi Makongoro hana sifa ya kuwa rais, kwani kuna vigezo gani vinavyoangaliwa? Angeomba ushauri kwanza hata kwa kina Butiku,” alisema Dk Bana.

Alisema kwa anavyofahamu, CCM huchagua viongozi wazalendo, wenye maadili na historia za kupendeza wala si viongozi kutokana na koo zao au umaarufu tu. Kadhalika Dk Bana alisema mchakato wa kumpata rais ajaye ni mgumu hivyo akaitaka CCM isikurupuke.

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Profesa Gaudence Mpangala alisema haoni tatizo kwa mtoto huyo wa muasisi wa Taifa kwa kuwa ana sifa zote za uongozi na hana sifa ya ‘uchafu.’

“Ukizungumzia usafi wa viongozi, hana neno. Anaweza kuwa kiongozi mzuri tu na pia ana haki kikatiba,” alisema.

Profesa Mpangala alisema licha ya watu kukosoa kuwa watoto wa viongozi wa zamani wanatengenezwa kuwa viongozi, lakini kama mtu ana sifa basi hana budi kugombea.

Advertisement