Mtoto wa mwigizaji Mashaka azungumzia kifo cha baba yake

Muktasari:

Abdallah Ramadhan, mtoto wa mwigizaji Ramadhani Ditopile ‘Mashaka’ aliyefariki dunia leo Jumamosi Oktoba 20, 2018 amesema baba yake alifikwa na umauti wakati akimsubiri muuguzi aliyetakiwa kumsindikiza Hospitali ya Mloganzila.


Dar es Salaam. Abdallah Ramadhan, mtoto wa mwigizaji Ramadhani Ditopile ‘Mashaka’ aliyefariki dunia leo Jumamosi Oktoba 20, 2018 amesema baba yake alifikwa na umauti wakati akimsubiri muuguzi aliyetakiwa kumsindikiza Hospitali ya Mloganzila.

 

Akizungumza na MCL Digital leo Abdallah amesema Mashaka alipata shinikizo la damu jana usiku na kukimbizwa katika hospitali ya Amana ambako alipewa rufaa ya matibabu kwenda Mloganzila.

 

Amesema wakiwa Amana hali ya Mashaka ilizidi kuwa mbaya na aliwekewa mashine ya kumsaidia kupumua.

 

“Leo asubuhi waliamua kumpa rufaa ya matibabu kwenda Mloganzila lakini bahati mbaya wakati wakimsubiri nesi afike kwa kuwa muda huo wauguzi walikuwa wakibadilishana muda wa kuingia na kutoka kazini, alifariki dunia,” amesema.

 

Amesema kwa muda baba yake hakuwa akionekana katika uigizaji kwa kuwa aliamua kupumzika baada ya kupata ugonjwa wa kupooza mwaka 2013.

 

“Kuna wakati alikuwa akichukuliwa kwenda kufundisha baadhi ya vikundi baada ya kupona ugonjwa huo uliokuwa ukimsumbua,” amesema Abdallah.

 

“Mbali na shinikizo la damu pia baba alikuwa akisumbuliwa na kisukari.”

 

Mashaka alijizolea umaarufu mwanzoni mwa miaka ya 2000 wakati akiigiza na kikundi cha sanaa cha Kaole kilichoibua waigizaji wengi maarufu nchini

 

Abdallah amesema msiba upo maeneo ya Ilala Bungoni na maziko yatafanyika kesho katika makaburi ya Tabata Kinyerezi.