Mtu na mpenziwe watuhumiwa kughushi cheti malipo ya korosho

Mtwara. Wakati baadhi ya wakulima wakianza kulipwa wilayani Newala, mtu na mpenzi wake wametiwa mbaroni kwa tuhuma za kughushi cheti cha malipo ya korosho.

Mkuu wa wilaya hiyo, Aziza Mangosongo akizungumza kwa simu jana alisema watuhumiwa hao walikamatwa juzi katika Kata ya Makonga baada ya kupatikana kwa taarifa kuhusu udanganyifu uliopo kwenye chama cha msingi (Amcos) cha Makonga.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni karani wa chama hicho, Asma Rajab na Mohammed Namkunga anayedaiwa kuwa mpenzi wake.

“Siku ya tukio, Namkunga alikwenda na viroba viwili vya korosho. Baada ya kufanikiwa kuviingiza, Asma aliandika kwenye cheti kuwa Namkunga amepeleka kilo 200 na kwa bei ya Sh3,300 angepata zaidi ya Sh600,000 kinyume cha sheria,” alisema Mangosongo.

Mkuu huyo wa wilaya alisema wananchi walitoa taarifa baada ya kuelezwa kwamba wakiona mtu analeta korosho kinyume cha sheria kwenye chama msingi wazijulishe mamlaka husika.

Akizungumzia mkakati huo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Geldius Byakanywa alisema kabla ya malipo, uongozi unajiridhisha wakulima wanaostahili.

Akizungumza na Mwananchi jana, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga alisema hadi juzi jioni, Serikali ilikuwa imewalipa wakulima 2,168 kutoka vyama sita vya msingi vya Mkoa wa Lindi.

Alivitaja vyama hivyo kuwa ni Mtama, Kitoviki, Mnazi Mmoja, Mtetesi na Mtafitekwa.

“Mpaka jana (juzi) jioni idadi ni hiyo ila watu wa benki walibadilisha utaratibu wakaona badala ya kulipa kutoka makao makuu wagawanye timu zao kwenda wilayani,” alisema Hasunga. Kuna vyama 617 vya ushirika wa korosho nchi nzima lakini kwa kuanza vilizingatiwa 50 na mpaka sasa 35 vimefanyiwa uhakiki na wakulima wa vyama sita wamelipwa.

“Kuanzia Jumatatu (leo) wakulima wengi wataanza kulipwa,” alisema waziri huyo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wakulima walisema bado hawajaingiziwa fedha za mauzo ya mavuno yao.

Mkulima wa Kijiji cha Naliendele, Shaibu Kafukutu alisema amepeleka zaidi ya kilo 1,000 katika chama cha ushirika na korosho zake kuhakikiwa hivyo anasubiri malipo.

“Ukilinganisha na mwaka jana, msimu huu mavuno yameshuka kwa sababu ya hali mbaya ya hewa,” alisema Kafukuta.

Alisema mwaka huu ameuza kilo 1,500 tofauti na mwaka jana alipouza kilo 3,000 wakati mwaka juzi alikuwa na kilo 4,000.

Mwenyekiti wa chama cha ushirika cha Kijiji cha Mbawala, Salim Nakudabi alisema uzalishaji umeshuka kwa kiasi kikubwa hali inayotishia kufikia malengo waliyojiwekea.

Alisema chama hicho kilikuwa na lengo la kukusanya tani 400 lakini mpaka sasa kimepata tani 200.

“Mpaka sasa hatujui hatima ya ushuru wa chama chetu. Hatujui kama tutaupata kwa wakati maana tumekopa. Unajua hapa tuna walinzi, wabebaji na vibarua. Wote tunawalipa kwa pesa hii. Ikifika hadi Desemba hatujapata, tutakuwa na wakati mgumu kiutendaji,” alisema.