Mtulia awataka wapinzani wawaache wanaotaka kuhamia CCM

Muktasari:

Mbunge wa Kinondoni (CCM) Maulid Mtulia amewataka wabunge wa upinzani kuwaacha huru wabunge wenzao kwa kuwa pilipili wasiyoila haipaswi kuwawasha

Dodoma. Mbunge wa Kinondoni (CCM), Maulidi Mtulia ameliambia Bunge kuwa kuna wabunge wa chama kimoja bungeni wanamlinda mbunge wa chama kisichowahusu akahoji hofu yao ni ipi.

Mtulia ametoa kauli hiyo leo jioni bungeni Novemba 15, 2018 wakati akichangia Muswada wa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha wa mwaka 2018.

Wakati Mtulia akitoa kauli hiyo, Mbunge Tandahimba (CUF), Katani Katani alikuwa amekaa mahali wanapokaa wabunge wa Chadema huku akizungukwa na wabunge kadhaa.

Wabunge waliokuwa wamemzunguka Katani ni David Silinde (Momba), Joseph Haule ‘Profesa J’ (Mikumi), Paschal Haonga (Mbozi) na Antony Komu (Moshi Vijijini).

Mtulia ameanza kwa kuwashukuru zaidi wabunge wa CCM kwa kuwapokea na hata kuunga mkono kwa Rais kumteua Mwita Waitara kuwa Naibu Waziri wa Tamisemi.

"Mmetupokea vizuri asanteni wabunge wenzetu wa CCM, nawashukuru wabunge walioamua kuja katika kipande hiki naamini wako salama, CCM oyeeeeeeeeee," amesema Mtulia.

Baada ya maelezo hayo akawataka wabunge wa upinzani kuwaacha wabunge wenye uamuzi kufanya uamuzi wao sahihi bila kutishiwa.

Leo asubuhi Katani aliingia bungeni na muda mwingi katika viwanja vya Bunge walionekana wakiwa na aliyekuwa Mbunge wa Temeke (CUF), Abdallah Mtolea ambaye ametangaza kujiuzulu na kuhamia CCM.