Mtwara waanza kuyahama makazi yao

Baadhi ya watu wakiwa eneo la uwanja wa ndege kufuatia tahadhari ya uwezekano wa kutokea kimbunga Kenneth. Picha na Haika Kimaro

Muktasari:

  • Baadhi ya watu katika maeneo mablimbali mjini Mtwara wameonekana wakihama na familia zao kwa kutumia  magari binafsi na wengine wakitembea kwa miguu na wengine kwa pikipiki zilizobeba abiria zaidi ya wawili maarufu kama mshkaki.

Mtwara. Baadhi ya wakazi wa mji wa Mtwara wameanza kuyahama makazi yao kuelekea nje ya mji kutokana na kimbunga Kenneth kinachotarajiwa kuikumba mikoa ya Kusini ya Tanzania ya Mtwara, Lindi na Mtwara kuanzia leo Alhamis Aprili 25, 2019.

Soma:

Wengi wao wameonekana wakiwa kwenye magari yao binafsi, pikipiki na wengine kwa miguu.

Wengi wao wanaelekea nje ya mjini wa Mtwara katika maeneo yaliyotajwa na Serikali kwa ajili ya kujihifadhi na kupata huduma za dharura.

Maeneo hayo ni pamoja na uwanja wa ndege wa Mtwara na eneo la kikosi cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kikosi cha Naliendele ambako watu wengi wanaonekana kuelekea huko.

Wakati wakihama, tayari mvua ndogo ndogo zimeshaanza kunyesha lakini watu wanaendelea na safari pasipokujali kulowana.

Akizungumza na Mwananchi, mkazi mmoja wa Mtwaramjini  aliyetaja jina moja la Annette amesema amelazimika kuyahama makazi yake kwa muda kutokana na hali ya tahadhari iliyotangazwa na Serikali.

“Nimeondoka na watoto wangu wote na sasa tunaelekea eneo la Naliendele kwa ajili ya tahadhari kama ilivyotangazwa kwa sababu hatuwezi kujua nini kitatokea,” amesema Annette.

Mkazi wa Shangani jirani na pwani ya bahari ya Hindi, Ester Mmari ambaye amehama bila mizigo, amesema ni vyema watu wakachukua tahadhari kwa ajili ya kunusuru maisha yao endapo tukio hilo litatokea.

“Makazi yangu yako jirani na bahari lakini majirani zangu wao wamehama wote jana usiku, sijabeba mzigo zaidi ya nyaraka zangu muhimu kama bima ya afya na vyeti ambavyo siyo vizito kuliko kuanza kuhangaika na mizigo,” amesema Mmari.

Mkazi wa Kiangu Rajabu Yusuph amesema anahama kwa sababu yamekuwa yakikumbwa na mafuriko mara kwa mara.

“Kiangu hatuko karibu na bahari, lakini ni sehemu ambayo hukumbwa na mafuriko mara kwa mara kwa hiyo tumelazimika kuhama ili kama mvua kubwa zitanyesha tunusuru maisha yetu,” amesema  Yusuph.