Mufti Zubeir azungumzia masheikh wa uamsho

Muktasari:

Mufti Zubeir alizaliwa mwaka 1953 katika Kijiji cha Kwamndolwa Old Korogwe mkoani Tanga.Amesoma Shahada ya Sharia na Uon-gozi wa Dini aliyoipata katika vyuo vya ndani na nje ya nchi ikiwamo Misri na Kenya (Mombasa). Awali, alisoma hadi darasa la nane mkoani Tanga.

Miaka sita tangu kukamatwa kwa masheikh 22 wa Jumuiya ya Uamsho Zanzibar na kuwekwa mahabusu, Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubeir amezungumzia kwa mara ya kwanza suala hilo.

Masheikh waliopo mahabusu ni Farid Hadi Ahmed, Jamal Swalehe, Nassoro Abdallah, Hassan Suleiman, Anthari Ahmed, Mohammed Yusuph, Abdallah Hassan, Hussein Ally na Juma Juma.

Wengine ni Saidi Ally, Hamisi Salum, Saidi Amour Salum, Abubakar Mngodo, Salum Ali Salum, Salum Amour Salum, Alawi Amir, Rashid Nyange, Amir Hamis Juma, Kassim Nassoro, Said Sharifu, Sheikh Mselem Ali Mselem na Abdallah Said Ali.

Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu kuelekea maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Mufti Zubeir anasema licha ya suala hilo kuwa mikononi mwa vyombo vya dola anaamini haki itatendeka.

Anasema ni vyema kuviachia vyombo hivyo viendelee na uchunguzi kwa weledi kwa kuwa kuviingilia si jambo sahihi na hakutafanikisha kupata ufumbuzi.

“Ninachoomba kwa vyombo husika ni kutenda haki. Kinachopaswa kufanyika kifanyike kwa wakati mwafaka ili kila mmoja apate haki yake,” anasema.

Mufti anasema kama ni upelelezi unapaswa kufanyika kwa kuzingatia haki za washtakiwa hao na wengine, ili hatimaye hatua stahili za utoaji haki zitekelezwe.

Kuhusu matukio ya utekaji katika jamii likiwamo la Desemba 6, lililomkuta mkuu wa Chuo cha Kiislamu Nyakato jijini Mwanza, Sheikh Bashir Gora, Mufti Zubeir anasema ambacho kinapaswa kufanywa na Bakwata ni kushauri.

Kwa nini Bakwata haitoi matamko

Mufti Zubeir anasema baraza hilo linafanya mambo makubwa yenye manufaa kwa jamii hususani kwa Waislamu zaidi ya kutoa matamko. Anasema kulingana na uzito wa majukumu ya baraza hilo halipaswi kuweka wazi kila kitu kinachofanyika ingawa yapo mengi ya maana.

“Hivi hao wanaokosoa wanataka kila jambo tuliweke wazi. Yaani tukikutana na kiongozi mkubwa kujadili au kushauri juu ya jambo fulani nyeti tutoke hadharani kueleza…hapana, hatuwezi kufanya hivyo,” anasema.

Hata hivyo, Mufti Zubeir anasema mara kwa mara inapobidi baraza akiwamo yeye wamekuwa wakitoa hadhari au kushauri, kukemea au kuelekeza mambo yenye manufaa kwa jamii.

Mikakati ya Bakwata

Mufti Zubeir anasema wamedhamiria kuanzisha shirika la maendeleo kwa ajili ya kujiimarisha kiuchumi.

Anasema kuanzishwa kwa Bakwata mwaka 1968, kumefanikisha mambo mbalimbali na sasa wanakusudia kuimarisha nguvu ya kiuchumi.

Mufti anasema miongoni mwa mambo waliyoyachukulia hatua tangu alipoingia madarakani ni kuwakusanya watalaamu wabobezi wa fani mbalimbali wakiwamo wa uchumi kwa ajili ya kuchanganua na baadaye kuja na mkakati wa kutekeleza mapendekezo ili kufanyiwa kazi.

Akizungumzia shirika hilo la maendeleo ya kiuchumi, Mufti Zubeir anasema kamati hiyo inajumuisha wataalamu wa uchumi wenye uzoefu kutoka taasisi na idara mbalimbali wakiwamo waliowahi kutumika serikalini.

“Lengo la kuanzishwa Bakwata ni kutaka kusaidia kusukuma mbele maendeleo ya jamii hususan ya Waislamu katika mambo mbalimbali ikiwamo uchumi. Wataalamu watashauri nasi tutafanyia kazi ushauri wao,” anasema.

Anasema Bakwata sasa inasimamia kaulimbiu ya “Jitambue, Badilika Acha Mazoea” ambayo ndani yake, inalenga kuleta mafanikio katika maeneo mbalimbali.

Kuhusu utendaji wa Serikali chini ya Rais John Magufuli, Mufti Zubeir anasema kumekuwa na mafanikio katika maeneo mbalimbali hususan ya kiuchumi na miradi mingi inatekelezwa jambo ambalo linapaswa kuungwa mkono kwa dhati.

“Tunashirikishwa katika mambo mbalimbali yanayoihusu jamii, tunashauri na kufanya kila linalopaswa kufanyika katika mazingira na wakati sahihi,” anasema.

Miaka 50 ya Bakwata

Kuhusu miaka 50 ya uwapo wa Bakwata, Mufti Zubeir anasema Waislamu wanajivunia mambo mengi yaliyofinikiwa ikiwamo kuwa na uhuru wa kushiriki harakati na shughuli za maendeleo.

“Waislamu wanashiriki shughuli za kiuchumi, elimu, wako huru kuabudu na mambo mengi yamekuwa yakifanyika kwa uratibu, uangalizi na usimamizi wa karibu wa baraza lao.

“Sasa tunajiongoza wenyewe hakuna raia wa kigeni anayetuendeshea chombo hiki, hayo ni mafanikio makubwa yanayopaswa kusemwa waziwazi,” anasema.

Mfumo wa madrasa

Mufti Zubeir anasema ili kwenda na kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia, utoaji wa elimu ya dini katika vyuo vya dini (madrasa) nao unatazamwa upya.

Alisema tayari mikakati imewekwa kuhakikisha utoaji wa elimu katika madrasa unakuwa katika mpangilio mzuri kwa kufuata mtalaa (syllabus).

“Kwa miaka yote tangu kuanzishwa kwake Bakwata haijawahi kuwa na madrasa kwa ajili ya elimu ya dini, ingawa imeanzisha shule nyingi za elimu ya sekyula. Sasa tunataka walimu wa madrasa (maustadhi) wapatiwe mafunzo yatakayowawezesha kufundisha kulingana na mabadiliko yanayotokea katika jamii.

“Tumeshaanzisha kitu kinachoitwa ‘Daru al Maarifa’ kupitia chombo hiki tunakusudia kuwapa maustaadhi ujuzi wa taaluma mbalimbali kama elimu ya teknolojia ya habari na mawasiliano, kuwafundisha lugha mbalimbali za kigeni. Tunakoelekea tutaanzisha mfumo wa elimu ya sekondari kwa miaka miwili (QT) ili kuwapa fursa ya kupata elimu ya sekyula kwa walioikosa,” alisema.

Kuhusu shughuli za kiuchumi, mbali na kuanzisha shirika la maendeleo pia amewaagiza makatibu wote kuhakikisha wanatafuta maeneo kwa ajili ya kushiriki shughuli za kilimo.

Anasema kilimo ni moja ya nyenzo za uchumi na kwamba, Bakwata imedhamiria kushiriki kikamilifu kufanikisha hilo.

“Binafsi mimi ni mkulima, nina mashamba sehemu mbalimbali kama Morogoro na nyumbani kwetu Tanga. Hivyo, suala la kilimo tutalipa umuhimu kwa ustawi wa jamii na maendeleo ya Waislamu,” anasema.

Madai ya kutumiwa na serikali

Mufti Zubeir anasema Bakwata ni chombo kinachojiendesha kwa uhuru kamili bila ya kuingiliwa na Serikali katika mambo yake.

Anasema kwa miaka yote tangu kuanzishwa kwake imeendelea kusimama katikati ya Waislamu na dola, ili kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa bila ya kuwapo unyonyaji, ukandamizaji au uporaji wa haki.

Hata hivyo, anasema kutokana na jukumu zito ililonalo lazima kufanya kazi kwa karibu na Serikali kwa kuwa ndiyo inayoratibu, kusimamia na kuongoza nchi.

“Katika uislamu tunasititizwa kuwa wazalendo kwa nchi zetu, kwa kuwa nchi hii ina serikali ni lazima tufanye nayo kazi kwa karibu ili kuhakikisha mambo yanakwenda sawa,” anasema.