Muhimbili yaokoa Sh1.3 bilioni za upasuaji wa watoto wenye matatizo ya kusikia

Daktari bingwa wa upasuaji wa magonjwa ya masikio na koo  Edwin Liyombo akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya upasuaji huo kushoto daktari Bamani uteni Kaimu Mkurugenzi huduma za upasuaji  Picha na Omar Fungo .

Muktasari:

  • Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imefanya upasuaji kwa watoto 10 waliozaliwa na tatizo la kusikia na kuwapandikizia kifaa cha kuwasaidia kusikia huku malengo yakiwa ni kuwahudumia watoto 24 kila mwaka.

Dar es Salaam. Watoto 10 waliozaliwa na tatizo la kutosikia wamefanyiwa upasuaji katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na kupandikizwa kifaa kitakachowasaidia kusikia (cochlea implant).

Hii ni mara ya pili kwa hospitali hiyo kufanya upasuaji huo kwa kushirikiana na mtaalamu wa upasuaji na upandikizaji wa kifaa cha kusaidia kusikia, Profesa Lobna kutoka Chuo cha Ain Shams cha Misri.

Akizungumza na vyombo vya habari leo Jumapili Novemba 18, 2018 daktari bingwa wa masikio na koo, Dk Edwin Liyombo amesema upasuaji huo uliofanyika leo unafanya idadi ya watoto walionufaika na huduma hiyo kufikia 21 tangu huduma hiyo ilipoanzishwa Juni, 2018.

"Tanzania imekuwa nchi ya kwanza kutoa huduma hii kupitia hospitali ya umma ambayo ni Muhimbili. Wenzetu Kenya, huduma hii inatolewa na hospitali binafsi na inagharimu Dola za Marekani 31,000 (Sh71.4 milioni)," amesema Dk Liyombo.

Daktari huyo amesema huduma hiyo inatolewa hapa nchini kwa gharama ya Sh37 milioni kwa mtoto mmoja ambapo wangeenda nje ya nchi, kila mtoto angehudumiwa kwa Sh100 milioni. Amesema watoto hao 21 wangepelekwa nje ya nchi, wangetibiwa kwa gharama ya Sh2.1 bilioni lakini MNH imeokoa Sh1.3 bilioni.

Mmoja wa wazazi wa watoto hao, Veronica Kiondo amesema aligundua mtoto wake ana tatizo akiwa na mwaka mmoja. Amesema kila alipokuwa akimsemesha, mtoto alikuwa akimtazama usoni.

"Baada ya upasuaji huu nina matumaini kwamba mwanangu atapona na kuendelea kucheza na wenzake. Alikuwa anatengwa na wenzake kwa sababu hawaelewani," amebainisha mzazi huyo kutoka Tanga.