Museveni: Siondoki ng’o madarakani

Kampala, Uganda. Rais Yoweri Museveni amewaambia viongozi wa vyama vya upinzani kwamba hana mpango wowote wa kuachia madaraka na wanapaswa kuacha kufikiria serikali ya mpito.
Alizungumza hayo wakati wa mkutano ulioandaliwa na Taasisi ya Majadiliano ya Vyama (IPO), ambao ulishirikisha viongozi wa vyama vyenye wawakilishi bungeni, katika mji mkuu wa Kampala.
Museveni, ambaye alisema alifurahia majadiliano, aliwaambia wapinzani wake kwamba hatafikiria suala la kuachia madaraka hadi atakapokuwa ameridhishwa kwamba "ustawi na mkakati wa kiusalama wa Afrika vimefikiwa".
"Ninawasikia watu kama Mao wakizungumzia juu ya serikali ya mpito, namna ambavyo wangependa kukaa mbele ya watazamaji na kumwona Museveni akikabidhi madaraka. Hicho ndiyo kitu muhimu zaidi kwake. Sidhani kwamba ni muhimu zaidi na ni nzuri anasema hivyo," alisema Museveni Alhamisi.
"Kwa hiyo, darasa la siasa, badala ya kuzungumza juu ya hatima ya Afrika, mnzungumzia juu ya mambo madogo - chaguzi, kwamba nani anakuwa nani. Ndiyo maana nimesema kama bado nitaendelea kuwa na nguvu, nitaendelea," aliendelea.
"Huu ndiyo mtazamo wangu: siyo kustaafu wakati masuala ya awali kwa nini Afrika karibu iangamie hayajashughulikiwa. Na ninyi mnashughulika na mambo madogo - chaguzi. Wale ambao mnawachagua, mnawachagua ili wafanye nini hasa? Hilo ndilo mnapaswa kujibu. Sina maslahi mengine katika siasa kwa sababu mimi ni mfugaji wa ng'ombe."
Museveni, ambaye utawala wake utatimiza miaka 33 ifikapo Januari 26, 2019, alikuwa akijibu taarifa iliyosomwa na Rais wa chama cha Democratic Norbert Mao
Katika hotuba yake, Mao alisema kwamba wanaota ndoto ili siku moja mtu aliyeko madarakani atakwenda kwenye viwanja vya Uhuru vya Kololo ili kushuhudia kuapishwa kwa mtu mwingine kuwa rais wa Uganda na kukabidhi rasmi mamlaka.
Museveni aliwaambia viongozi kuwa ikiwa bado wanamfikiria yeye kuondoka ikulu hivi karibuni, "ni bora waanze kuota mambo mbadala”.