Muswada wa vicoba, saccos wagonga mwamba bungeni

Dodoma. Kamati ya Bunge ya Bajeti imeurudisha serikalini Muswada wa Huduma Ndogo za Fedha wa mwaka 2018 uliokuwa usomwe kwa mara ya pili bungeni jana.

Bila kutaja sababu za kuurudisha muswada huo, Naibu Spika, Dk Tulia Ackson alitangaza kuahirisha kikao baada ya kipindi cha maswali na majibu asubuhi.

Alipoulizwa nje ya Bunge na Mwananchi juu ya sababu za kutowasilishwa kwa muswada huo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alijibu kwa kifupi kuwa hana sababu.

Hata hivyo, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji alisema wangekutana na kamati hiyo saa 7.00 mchana jana kwa ajili ya majadiliano na baada ya hapo ndipo angeweza kuwa na jambo la kusema.

Alipoulizwa iwapo kuna vifungu ambavyo hawajakubaliana na Serikali, mwenyekiti wa kamati hiyo, George Simbachawene alisema walikuwa katika majadiliano na hawezi kutoa vitu nusunusu.

Novemba 5, wakati Spika Job Ndugai akieleza kuhusu shughuli za mkutano wa 13 wa Bunge, alisema muswada huo umeletwa kwa hati ya dharura.

Ulipowasilishwa bungeni ulisomwa kwa mara ya kwanza Novemba 6 na kupangiwa kusomwa mara ya pili jana, kabla ya kujadiliwa na kupigiwa kura ya uamuzi leo, jambo ambalo halijatimia kama lilivyopangwa.

Juzi, kamati hiyo ilikutana hadi usiku wa manane kuuchambua muswada huo ambapo mmoja wa wajumbe alilieleza Mwananchi kuwa, muswada huo haujaishirikisha Zanzibar, hivyo kusababisha mvutano kati ya wabunge na Serikali.

Pia, alisema kifungu kingine kinachotaka vicoba kusajiliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kilipingwa na wabunge wengi waliotaka kiondolewe kwa sababu vingi vinaundwa kwa lengo la kusaidiana na siyo kibiashara.