Mwale apigwa faini Sh200 mil, mali zake zawekwa kiporo

Muktasari:

  • Watuhumiwa wengine wawili waliobaki kwenye kesi hiyo ni mameneja wa Benki ya CRDB Arusha, Boniface Mwimbwa na Elias Ndejembi ambao kesi zao zinaendelea baada ya kukana kuhusika na makosa ambayo yanawak-abili na kesi yao imepangwa kusomwa Desemba 15.02

Arusha. Jaji Issa Maige wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha jana aliweka kiporo uamuzi wa kutaifisha mali za Wakili Medium Mwale, lakini akamhukumu kifungo cha miaka mitano jela au kulipa faini ya Sh200 milioni baada ya kumtia hatiani kwa makosa ya utakatishaji fedha.

Akisoma hukumu hiyo iliyochukuwa takriban saa moja-- kuanzia saa 4:46 asubuhi--, Jaji Maige alisema maombi ya upande wa mashitaka yaliyowasilishwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Oswald Tibabyakyomya kutaka kuifisha mali za Mwale alizopata kinyume cha sheria, linapaswa kusubiri utaratibu.

Alisema ingawa kifungu cha 251 cha sheria ya utakatishaji fedha kinaruhusu kutaifishwa kwa mali zilizopatikana kinyume cha sheria, kifungu kidogo cha tatu cha sheria hiyo kinatoa nafasi kwa mahakama kuzingatia utaratibu.

Jaji Maige alisema kifungu cha 28 cha sheria hiyo, pia kinataka kuzingatiwa taratibu katika kutaifishwa mali, ikiwamo kuwasilishwa mahakamani maombi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Hukumu ya Mwale

Jaji Maige alisema kutokana na makosa 17 ya Kugushi yaliyokuwa yakimkabili, anamuhukumu Mwale kwenda jela miaka saba jela, lakini kwa sababu tayari alishakaa kizuizini kwa miaka hiyo, hivyo hataitumikia tena.

Pia, alisema katika makosa matano ya kuandaa nyaraka za uongo, amemuhukumu kifungo cha miaka miwili na kosa la kula njama ambalo ni kinyume na kifungu cha 384 cha kanuni ya adhabu, kifungo cha miaka mitano jela.

Hata hivyo, Jaji alisema katika namba 1 na 29, ambayo yanahusu makosa ya utakatishaji fedha, mahakama imemuhukumu kulipa faini ya Sh100 milioni kwa kila kosa na akishindwa atumikia kifungo hicho.

Hata hivyo, alisema kwa kuwa Mwale tayari amekuwa kizuizini kwa miaka saba, tayari ametumikia adhabu ya kifungo cha jumla cha miaka saba.

Baada ya uamuzi huo, Mwale alirejeshwa mahabusu kusubiri kukamilisha taratibu za kulipa faini na kutoka gerezani.

Akisoma hukumu hiyo, Jaji Maige alisema mahakama imetoa hukumu kwa kuzingatia kuwa, mshitakiwa amekiri makosa na hana kumbukumbu za uhalifu.

Alisema mshitakiwa ameokoa muda wa mahakama kuendelea na shauri hilo, kwa sababu upande wa mashtaka ulipanga kuita mashahidi 59 wa ndani na nje ya nchi na vielelezo 64.

Jaji Maige pia alisema kukiri kosa kumeondoa kukwepa adhabu kiufundi, lakini kwa kuwa hili ni kosa la kwanza, ni wazi ameungama na atajirekebisha.

Alisema pia hukumu hiyo, imezingatia kuwa mtuhumiwa anategemewa na mama mzazi mwenye miaka 78 na mtoto wa miaka minane.

Watuhumiwa wengine wawili kwenye kesi hiyo ni Boniface Mwimbwa na Elias Ndejembi ambao kesi zao zinaendelea baada ya kukana kuhusika na makosa ambayo yanawakabili.