Mwijage aanza kuwapigania wananchi wake bungeni

Mbunge wa Muleba Kaskazini (CCM), Charles Mwijage  akiuliza swali kwa mara ya kwanza bungeni jijini Dodoma leo, tangu uteuzi wake katika nafasi ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji ilipotenguliwa na Rais John Magufuli.

Muktasari:

  • Aliyekuwa waziri wa viwanda, biashara na uwekezaji, Charles Mwijage leo ameuliza swali kwa mara ya kwanza bungeni tangu alipoondolewa kwenye nafasi ya uwaziri wiki iliyopita

Dodoma. Mbunge wa Muleba Kaskazini (CCM), Charles Mwijage ameitaka Serikali kuharakisha inapeleka umeme katika jimbo lake ili wananchi wanufaike na miradi ya umeme vijijini (Rea).

Mwijage ambaye alivuliwa nafasi ya uwaziri wa viwanda, biashara na uwekezaji wiki iliyopita, kabla ya kuuliza swali bungeni leo, alimshukuru Rais John Magufuli, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na uongozi wa Bunge kwa namna walivyompa ushirikiano wakati wote wa utendaji kazi na viongozi wa dini wanaomuombea wakati wote.

Mbunge huyo huku akishangiliwa, alisema wananchi wake walipata mradi wa umeme katika jimbo zima lakini maeneo mengi yaliishia kuwekwa mambo bila ya kusimikwa kwa nguzo.

"Ni lini sasa Serikali itawaondolea kero ya umeme ili wananchi wale nao waanze kunufaika na miradi ya Rea," alisema Mwijage

Akijibu swali hilo, Waziri wa Nishati,  Dk  Medard Kalemani alisema miradi ya umeme katika wilaya ya Muleba itatekelezwamuda si mrefu na mkandarasi yuko katika maandalizi ya kupeleka nguzo.