NHC yakabidhi hatimiliki na kibali cha ujenzi kwa AUWSA.

Muktasari:

Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limekabidhi hatimiliki na kibali cha ujenzi kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (AUWSA) katika eneo la Safari City lililopo Mateves -Kisongo kwa ajili ya ujenzi wa ofisi kuu na ofisi ya kanda.

Arusha. Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limekabidhi hati miliki na  kibali cha ujenzi kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (AUWSA) katika eneo la Safari City lililopo Mateves -Kisongo kwa ajili ya ujenzi wa ofisi kuu na ofisi ya kanda.

Akikabidhi hati hiyo kwa kaimu meneja wa AUWSA leo, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Maulidi Banyani alisema wamekuwa na mahusiano mazuri kati yao na AUWSA na kwamba uwapo wa ofisi hizo utaharakisha shughuli za maendeleo katika eneo hilo.

Alisema eneo la Safari City ambalo limejengwa mradi wa nyumba mbalimbali za makazi na biashara litasaidia kupunguza msongamano ndani ya jiji la Arusha.

Alisema NHC imefanya mazungumzo na mamlaka hiyo kwa ajili ya ujenzi wa ofisi hiyo ikiwa na lengo la kuuendeleza mji huo kuwa wa kisasa zaidi.

"Tunaomba sana wale wote waliopatiwa maeneo haya waanze maendelezo haraka ili kuharakisha utoaji wa huduma mbalimbali katika eneo hili na tunategemea ushirikiano zaidi kutoka mamlaka zote zilizopo jijini hapa," alisema.

Naye Kaimu Meneja wa AUWSA, Humphrey Mwiyombela alisema ujenzi wa ofisi hizo utagharimu zaidi ya Sh7 bilioni ukihusisha jengo kubwa la ofisi ili kuharakisha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuwafikia kwa haraka zaidi.

Alisema ujenzi huo wa ofisi kuu ya mamlaka hiyo na ofisi ya kanda utajengwa kwa mfumo wa ghorofa sita.

Naye mwenyekiti wa bodi ya AUWSA, Dk Richard Masika alisema wamejiwekea mikakati kuhakikisha wanafikia wananchi kwa asilimia 100 ifikapo mwaka 2020 kama ambavyo dhamira ya Serikali ya awamu ya tano ilivyo ya kuhakikisha wanamtua mama ndoo ya maji kichwani.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Richard Kwitega aliipongeza NHC kwa kuanzisha mradi huo ambao utaondoa msongamano jijini Arusha na kuzitaka taasisi zingine kupeleka huduma zao katika eneo hilo ili kuharakisha maendeleo.