NMB yatoa msaada wa mabenchi 52 Muhimbili

Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee an watoto, Dk Faustine Ndugulile akizungumza baada ya kupokea mabenchi 52 ya kukalia jamaa na ndugu wanaosindikiza  wagonjwa katika kitengo cha matibabu ya dharura katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Kushoto ni Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Badru Idd na Katikati ni Mkuu wa Idara ya wagonjwa wa dharura na ajali Dk Juma Mfinanga

Muktasari:

  • Benki ya NMB imetatua changamoto ya mabenchi katika idara ya dharura (EMD) ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).

Dar es Salaam. Benki ya NMB leo imetoa msaada wa mabenchi 52 zenye thamani ya Sh10 milioni kwa idara ya dharura ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).

Akikabidhi msaada huo leo Desemba 9, 2018 meneja wa benki hiyo Kanda ya Dar es Salaam, Badru Idd amesema msaada huo ni sehemu ya benki hiyo kurudisha shukurani kwa jamii.

“Kama ilivyo ada kila mwaka tunatumia asilimia moja ya faida yetu kurudisha kwa jamii hususan katika afya, elimu na majanga. Kwa ujumla ni mambo yote ambayo yanaongeza mzigo kwa wateja wetu na Watanzania,” amesema Idd.

Kaimu mkurugenzi wa huduma za matibabu wa MNH, Dk John Rwegasha  ameshukuru kwa msaada hao akisema mabenchi hayo yatawasaidia wagonjwa wanaosubiri huduma na ndugu wanaokuwa wamewasindikiza.

“Tunashukuru kwa msaada huu na tunataraji NMB itaendelea na juhudi hizi kwani hospitali yetu inakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinahitaji utatuzi, kwa kuwa tangu kuanzishwa kwa kitengo hiki cha dharura hakukuwahi kuwa na mabenchi,” amesema Dk Rwegasha.

Naye Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile ambaye alihudhuria makabidhiano hayo alisema NMB ni benki inayofanya vizuri kuwafikia Watanzania  na kuwasaidia katika mambo mbalimbali.

“NMB Mmekuwa mkifanya vizuri kuwafikia watu wengi lakini mnapaswa kuongeza juhudi zaidi kufikia maeneo yote nchini, kwani kuna mahali ambako watu hawajajumuishwa kwenye huduma za fedha,” amesema Dk Ndugulile.