Nape: CCM kuna wasakatonge

Nape: CCM kuna wasakatonge

Muktasari:

CCM kimewataka wananchi kutotumia vibaya mitandao ya kijamii, huku kikikanusha taarifa zilizosambaa katika mitandao hiyo zikimnukuu Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Bashiru Ally kumjibu aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.

Dar es Salaam. Sakata la waziri wa zamani wa mambo ya nje, Bernard Membe, lililohusisha mitandao ya kijamii, bado halijapoa; jana ilikuwa zamu ya Nape Nnauye na CCM.

Wakati Nape akizungumzia akaunti ya Twitter iliyomuhusisha na mipango ya kuanzisha chama kipya cha Usawa kwa kushirikiana na Membe, CCM ilitoa tamko kukemea akaunti ya mtandao wa kijamii iliyotumia jina la Dk Bashiru kumjibu waziri huyo wa zamani.

Dk Bashiru alianzisha sakata hilo wakati akizungumzia umuhimu wa mshikamano ndani ya CCM, akisema ameshaongea na wanachama wote waliojitokeza kugombea urais mwaka 2015, isipokuwa Membe.

Alisema amesikia taarifa kuwa Membe anakwamisha harakati za Rais John Magufuli za mwaka 2020 na kwamba ameanza vikao kujiandaa kugombea na hivyo anamtaka aende ofisini kwake akajitetee.

Membe hakujitokeza hadharani kumjibu, lakini akaunti ya Twitter iliyokuwa na jina lake ikasema ataitikia wito na kutaka mtu aliyetoa tuhuma hizo awepo siku atakayokwenda, lakini Dk Bashiru akasema huo si utaratibu wa CCM.

Jibu hilo lilimuibua spika wa zamani, Pius Msekwa ambaye alimkosoa Dk Bashiru kabla ya yeye mwenyewe kukosolewa na katibu wa zamani wa chama hicho, Yusuf Makamba.

Jana akaunti nyingine ya Twitter ilijitokeza ikiwa na jina la “Sauti ya Kisonge”, ikieleza mpango huo wa kuanzisha chama kipya kinachohusisha vigogo wa zamani pamoja na Membe na Nnauye.

“Niliposoma upuuzi huu sasa ninaamini CCM imevamiwa na wasaka tonge wasiojua imani wala itikadi ya chama. Hawana wanachoamini isipokuwa matumbo yao! Uongo huu ni kwa faida ya nani? Watatoka wao, wenye chama tupo sana!” ameandika Nape katika akaunti yake ya Twitter akiambatanisha na ujumbe huo wa Sauti ya Tonge.

Alipotakiwa kufafanua, Nape alisema: “Kama mtu anaweza kutunga uongo ili kumchafua mtu maana yake hawajali chama hao.”

CCM nayo ilijiweka mbali na akaunti yenye jina la Dk Bashiru, ikiwaelezea waliofanya hivyo kuwa ni watu “wenye hila, fitna, husuda na kila chembe ya uzandiki” na ambaye “wametengeneza kauli ya kubeza, potofu na isiyo na ukweli”.

“Kwa utaratibu wa CCM, msemaji ni mmoja ambaye ni mwenyekiti. Kwa chama anayepewa dhamana ya kusema ni katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, mwenye dhamana ya itikadi na uenezi na si vinginevyo,” alisema katibu huyo wa uenezi na itikadi, Humphrey Polepole.