Nape, Zitto wazungumzia korosho

Dodoma/Dar. Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye amesema ni matumaini yake sakata la korosho litatumika kama mafunzo na kujipanga ili misimu inayokuja kuliepusha Taifa kupita kwenye mawimbi yanayofanana na ya mwaka huu.

Akichangia Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2019/20, bungeni jana Nape aliwashukuru wakulima kwa utulivu walioonyesha katika kipindi alichokiita ni cha milima na mabonde waliyopitia.

Mbali ya Nape, taarifa iliyotolewa jana na Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe inasema uamuzi huo wa Serikali ndiyo ulikuwa msimamo wake tangu awali.

“Tunakaribisha uamuzi wa Serikali wa kununua kwa bei nzuri korosho zote za wakulima kama tulivyopendekeza,” amesema Zitto katika taarifa hiyo akirejea mkutano wake na vyombo vya habari uliofanyika Oktoba 28.

Katika mkutano huo, Zitto alisema alitaka: “Serikali inunue korosho yote kwa wakulima ili kuwalinda na bei ndogo kutokana na kushuka kwa bei kwenye soko la dunia.”

Uamuzi huo wa Serikali pia umepongezwa na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) ambayo ilisema inampongeza Rais kwa hatua ya kuwalinda wakulima ambao nao ni sekta binafsi iliyojikita katika kilimo.

Wanunuzi walia

Wakati Nape, Zitto na TPSF wakipongeza, baadhi ya wafanyabiashara wamesema uamuzi wa Rais John Magufuli wa kuagiza Serikali inunue korosho zote kwa wakulima, unaathiri biashara yao.

Mkurugenzi mwenza wa Kampuni ya OM Agro, Mashaka Msumali akizungumza kwa simu jana alisema, “Kampuni yetu ilikuwa kwenye mchakato wa kununua tani 5,000 kwa Sh3,100 lakini sasa mipango hiyo imekufa kwa sababu Rais amesema hata walioandika barua kwa Waziri Mkuu nao wamechelewa na hawataruhusiwa kununua korosho kwa msimu huu.”

Alisema tayari kampuni yake ilikuwa imekodi maghala ya kuhifadhia korosho na wafanyabiashara wengine wamechukua mikopo kwenye benki hivyo ni hasara kwao na na wasafirishaji.

Meneja wa masoko na mauzo wa kampuni ya Hawte Investment Ltd, John Joseph alisema walishapokea oda ya zaidi ya tani 12,000 na sasa wanafanya mchakato wa kuisitisha.

“Itatubidi tusubiri fursa waliyoisema kwa wabanguaji wa ndani,” alisema.

Imeandikwa na Sharon Sauwa na Peter Elias, Ephrahim Bahemu.