Ndege ya sita Serikali kutua Tanzania kesho

Muktasari:

Ndege nyingine mpya aina ya Airbus A220-300 inatarajiwa kuwasili nchini kesho Ijumaa Januari 11, 2018 mchana ikitokea Canada, na Rais John Magufuli anatarajia kuongoza mapokezi ya ndege hiyo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam (JNIA)

 


Dar es Salaam. Ndege nyingine mpya ya Serikali aina ya Airbus A220-300 iliyopewa jina la Ngorongoro inatarajia kuwasilini nchini kesho Ijumaa mchana, ambapo itafanya idadi ya ndege zilizonunuliwa na Serikali kufikia sita.

Ndege hiyo ambayo tayari inanakshi za Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) endapo itakodishwa kwa shirika hilo kama ilivyofanyika kwa ndege nyingine tano itafanya jumla ya ndege za ATCL kufikia 7, ikijumlishwa na ndege yao ya zamani aina ya Bombardier Q300 ambayo sasa ipo katika matengenezo.

Ndege inayotarajiwa kutua kesho ni ya pili ya aina hiyo, kwani Desemba 23 iliwasili ya kwanza ambayo ilipewa jina la Dodoma. Ndege nyingine zinazomilikiwa na shirika hilo ni Bomberdier Q400-8 tatu na Boeing 87-8 (Dreamliner) moja.

Tangu Serikali ya awamu ya tano iingie madarakani Novemba 5, 2015 imekuwa ikipigania kulifufua shirika hilo ambalo ilikuta likitawala soko la ndani kwa asilimia mbili likiwa na ndege moja aina Bombardier Q300, lakini tangu kuongezwa kwa ndege hizo ukubwa wake wa soko uliongezeka na kufikia asilimia 31 mpaka Septemba mwaka 2018.