Ndoto ya Kagame inavyoigeuza Bandari

Muktasari:

  • Mkataba wa dola 154 milioni za Kimarekani baina ya TPA na China Habour Engineering Company Ltd unahusu upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam kwa kuongeza kina cha magati kutoka mita 8 hadi 15 kuwezesha meli zinazobeba mzigo wa hadi tani 19,000 kutia nanga na utakamilika ndani ya miezi 36.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) imesema inasuka upya idara zote ikiwa ni mkakati wa kutaka njia hizo za uchumi ziendeshe nchi.

Mpango huo unaenda sambamba na matamanio ya Rais Paul Kagame, ambaye nchi yake ya Rwanda haijapakana na bahari, aliyewahi kusema kwamba bandari pekee inatosha kulisha nchi.

Mkurugenzi mkuu wa TPA, Deusdedit Kakoko alisema jana kuwa, mbali na kutangaza nafasi 68 kuanzia za wakurugenzi hadi maofisa wa kawaida, mamlaka hiyo inabadilisha miundombinu, kuimarisha ulinzi na usalama na kufanya kampeni za masoko na uhusiano mwema ili kufikia malengo ya bandari kwa asilimia 100.

Pia wanarasimisha bandari bubu zaidi ya 250 kote nchini ambazo zinafanya kazi kinyume na utaratibu na kuikosesha Serikali mapato, ili ziweze kuwa kwenye utaratibu.

TPA inaendesha bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara zilizo katika Bahari ya Hindi, na nyingine zilizo Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa.

Kati ya bandari hizo, Dar es Salaam inapokea karibu asilimia 90 ya mizigo yote.

Kwa takriban miaka mitatu, viongozi wa juu wa Serikali, hasa Rais John Magufuli na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, wamekuwa wakifanya ziara za kushtukiza bandarini na kubaini wizi, ukwepaji kodi na ushuru, mizigo kutelekezwa, udhaifu katika udhibiti wa mafuta na upotevu wa makontena.

Akizungumza na baadhi ya vyombo vya habari nchini jana, Kakoko alisema kama alivyowahi kusema Rais Kagame bandari peke yake inatakiwa kulisha nchi. Alisema juhudi zimeanza miaka miwili iliyopita tangu Rais Magufuli alipoingia madarakani.

“Tunafanya mageuzi ya kutosha hasa kwenye rasilimali watu ndiyo maana tunahitaji watu ambao tumetangaza nafasi zao,” alisema Kakoko.

Kakoko alisema katika kurekebisha miundombinu, wanajenga magati hadi namba saba katika Bandari ya Dar es Salaam ili kuruhusu meli kubwa kutia nanga.

Alisema gati namba sifuri linaloitwa roro(roll in roll out) hadi namba saba ujenzi wake umefikia asilimia 25 sasa na ifikapo Juni, 2020 yatakuwa yamekamilika yote na kuendelea na gati namba nane hadi 18.

“Gati namba moja tayari limekamilika na litaanza kufanya kazi. Kinachomaliziwa ni kufunga mipira mikubwa kwa ajili ya meli kuweza kutia nanga,” alisema.

“Tunatakiwa ifikapo 2021 tuwe tunaweza kuhimili tani milioni 21 kutoka milioni 16.2 za sasa.”

Alisema katika ukaguzi walibaini bandari bubu zaidi ya 250 na bado wanaendelea kukakugua bandari hizo kwa kuwa wanahisi zinaweza kuwa na mapato yanayofikia nusu ya kinachopatikana Dar es Salaam.

“Hizi bandari hazitoi mapato ndiyo tumeshtuka na tunaangalia jinsi ya kuzirasimisha kwa utaratibu na kuhakikisha suala la usalama upo kwa kuwa ni nyeti kwenye bandari,” alisema.

Alisema huenda silaha zikawa zinapitishwa kwenye bandari bubu na ndiyo maana suala la usalama ni muhimu.

“Tunataka kushirikiana na serikali za mitaa, vijiji, wilaya na mkoa ili zoezi hili la urasimishaji liwe shirikishi na ili kujua huko ziliko kama wanazitambua,” alisema Kakoko.

Alisema bandari hizo ziko katika wilaya zaidi ya 20 nchini na ndiyo maana wamewahusisha viongozi wa maeneo hayo ili kurekebisha makosa yaliyofanyika miaka mingi iliyopita.