Ndugai ataja mbinu mpya ushindani

Dodoma. Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema matumizi pekee ya Kiswahili katika kufundishia shuleni yataendelea kuitupa nje Tanzania katika soko la ushindani.

Amesema wakati Taifa linaendelea kung’ang’ania kutumia Kiswahili nchi zingine zimechagua lugha zaidi ya tatu na zinafundishwa kuanzia ngazi ya chini.

Ndugai alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki katika mkutano wa wadau wa elimu wa Mkoa wa Dodoma, akisema dunia imepanuka hivyo kuendelea kutumia lugha moja itakuwa ni kupoteza muda.

Alisema malalamiko yataendelea kuwepo kwamba Watanzania hawana thamani katika soko la kimataifa wakati hawaandaliwi kushindana, bali wanaandaliwa kuwa walalamikaji.

“Hata hapo Rwanda wanafundisha Kiingereza, Kifaransa, Kinyarwanda na Kiswahili wakati sisi tunatangaza Kiswahili tu, haipo hiyo, nasema haipo tutaendelea kulalamika kila mahali kama hatuwezi kubadilika,” alisema Ndugai.

Mbunge huyo wa Kongwa alisema lugha hiyo siyo mbaya kufundishia, lakini Wizara ya Elimu inaweza kuangalia kama itafaa ili waruhusu lugha zingine kufundishwa shuleni au vyuo vitakavyoweza kwa ajili ya kuzalisha wasomi watakaomudu ushindani.

Katibu tawala wa Mkoa wa Dodoma, Kessy Maduka alisema ushauri huo unaweza kufanyiwa kazi na wahusika.