VITA YA KAGERA: Nyerere aipuuza OAU, aamuru jeshi liingie Uganda - 9

Muktasari:

  • Jana Uganda ilipovamiwa na makomandoo wa Israel katika kile killichoitwa ‘Operation Entebbe’ au kama ilivyojulikana kwa wengine, ‘Operation Thunderbolt’, Jumapili ya Julai 4, 1976 na ndege zake za kijeshi kuharibiwa vibaya, Urusi iliahidi kuimarisha kikosi cha anga cha jeshi la nchi hiyo na kuwapa ndege nyingine za kivita. Kwa ahadi hiyo uhusiano kati ya Uganda na Urusi ukaanza kuimarika tena. Marubani wa ndege za jeshi za Uganda walipelekwa mafunzoni Urusi.

Miongoni mwa hao ni Luteni David Omita, Luteni Atiku na Luteni Abusala ambao baadaye walikuja kuwa marubani wa kwanza kuishambulia Tanzania kwa ndege za kivita.

Pamoja na uhusiano huo kati ya Uganda na Urusi, wote hawa Urusi na nchi nyingine za Ulaya Mashariki walisema wako tayari kuendelea kuipa Uganda silaha na zana zingine za kijeshi, lakini sharti lilikuwa ni kulipa kwa fedha taslimu na si kwa mkopo.

Uingereza na Ujerumani Magharibi kwa upande wa Tanzania zilitoa msaada katika vita hiyo kwa njia isiyo ya moja kwa moja kwa kutoa mamilioni ya dola kusaidia wakimbizi wa Kagera.

Kwa hiyo fedha ya Tanzania iliyokuwa itumike kwa wakimbizi hao ikatumika vitani badala yake. Canada ilikuwa ikitoa silaha kwa Tanzania zikiwamo ndege za kivita na kwa mujibu wa vyanzo fulani, hata baadhi ya marubani wa ndege za jeshi walipokea mafunzo yao nchini Canada.

Muda mrefu hata kabla ya vita kuanza, Tanzania ilikuwa imeagiza ndege zake kutoka Canada. Wakati vita ilipozuka, kwa mujibu wa kitabu cha War in Uganda, Tanzania ilijaribu kuiharakisha Canada itume ndege hizo. Lakini Canada haikufanya lolote. Hata hivyo ndege hizo zilifika baada ya vita kumalizika. Kuhusu upatikanaji wa silaha nchini Uingereza, kitabu hicho kinaandika kuwa Tanzania ilimtegemea sana Amin Kashmiri ambaye wakati vita inaanza alikuwa London, Uingereza, akifanya kazi ya uwakala wa ununuzi wa silaha kwa ajili ya Tanzania na nchi nyingine za Afrika.

Kashmiri au kama wengine walivyomuita Sheikh Mohamed Ameenullah Kashmiri, ilikuwa ateuliwe kuwa mkuu wa majeshi katika mabadiliko ya uongozi jeshini ya mwaka 1974, lakini iliaminika kuwa hakupewa wadhifa huo kwa sababu ya asili yake ya India.

Wasifu wake unaonyesha kuwa Luteni Kanali Kashmiri alizaliwa mwaka 1935 mkoani Tabora na kusoma Shule ya Sekondari ya Karimjee ya Tanga (1950-1956) na baadaye chuo cha kijeshi cha Royal Academy Sandhurst nchini Uingereza (1958 - 1960).

Yeye na Mrisho Sarakikya ndio walioshiriki kikamilifu kulisuka upya Jeshi la Tanzania mara baada ya uasi wa Januari 1964.

Hata hivyo, Serikali ya Uingereza haikutaka kujihusisha waziwazi katika mgogoro wa Tanzania na Uganda. Lakini angalau vifaa vya kujenga upya daraja la Mto Kagera vilitolewa na Uingereza.

Kashmiri alifanikisha kupatikana kwa mabuti ya jeshi, mahema na baadhi ya vifaa vingine, na vikapakiwa kuletwa Tanzania.

Kupita kote huko duniani ni katika Afrika tu ndiko ambako Tanzania ilipata marafiki wa kweli. Msumbiji na Zambia walitoa hadharani taarifa za kumlaani Idi Amin kuivamia Tanzania.

Msumbiji ilitoa kikosi cha wapiganaji wake kwenda vitani Kagera, nchi za mstari wa mbele nazo kila moja zikachangia silaha. Algeria nayo ilituma meli tatu za silaha.

Lakini katika yote hayo, walioiokoa Tanzania kwa maana ya zana za kivita ni silaha za Jeshi la Uganda.

Wanajeshi wa Uganda walipokuwa wakiwakimbia wapiganaji wa JWTZ waliacha silaha nyingi nyuma yao ambazo JWTZ ilizikusanya na kuzitumia. Shida kubwa ya Tanzania ikawa si silaha tena, bali ni namna ya kusafirisha silaha walizopata. JWTZ ilikusanya silaha nyingi sana za jeshi la Idi Amin kiasi kwamba kuliibuka utani kuwa “Idi Amin alikuwa mgavi mkuu wa silaha kwa Tanzania.”

Awamu ya kwanza ya Vita vya Kagera ikawa imemalizika kwa kuyafukuza majeshi ya Idi Amin katika ardhi ya Tanzania.

Lakini Rais wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere hakuridhika tu na kuwaondoa katika ardhi yake kwa sababu aliamini akiwaacha watashambulia tena.

Baada ya kuwaondoa katika ardhi ya Tanzania kilichofuata ilikuwa ni uamuzi mgumu— kuwaandama hadi ndani ya Uganda kwenyewe ili kuhakikisha hawabaki kuja kushambulia tena. Lakini Nyerere alikuwa kwenye shinikizo kubwa kutoka kwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) wakimtaka asitishe vita dhidi ya Uganda.

Aliyekuwa mwenyekiti wa OAU, Rais Jaafar Nimeiry wa Sudan, alianza kumkaba Rais Nyerere kuhusu vita ya Uganda akimtaka ayaondoe majeshi yake. Nyerere naye alimshutumu Nimeiry na OAU kwa kushindwa kulaani uvamizi wa Amin na kutaka kusitisha mapigano wakati Amin akiwa ameikalia ardhi ya Tanzania.

Nyerere alitangaza hadharani kuwa hafikirii kusitisha vita dhidi ya Uganda hadi awe na uhakika na usalama wa Tanzania. Msimamo huo alianza kuuonyesha siku ile alipotangaza vita, Alhamisi ya Novemba 2, 1978. Katika hotuba yake, Mwalimu Nyerere alisema: “...Marafiki zetu wanaotuomba maneno ya suluhu waache maneno hayo. Kuchukua nchi ya watu wengine si kwamba majeshi yamekosea njia na kusema kuwa sasa sehemu hiyo umeichukua na kutangaza vita kwa nchi ile nyingine. Si sisi tuliofanya hivyo. Amefanya hivyo mwendawazimu.

“Sasa rafiki zetu, kama ni marafiki wa kweli, watataka tumwondoe mtu huyu. Hawawezi kutuomba suluhu au jambo la ajabu kabisa turudishe majeshi yetu nyuma. Niyarudishe wapi?”

Nigeria, ambayo huenda bado ilikuwa imekasirishwa na kitendo cha Tanzania kuitambua Biafra iliyojitenga nayo ilionyesha msimamo wake waziwazi dhidi ya Tanzania juu ya Vita vya Kagera.

Biafra ilijitenga na Nigeria Jumanne ya Mei 30 1967. Mwaka uliofuata, Jumamosi ya Aprili 13, 1968, Nyerere akaitambua.

Mkuu wa Jeshi la Nigeria, Luteni Jenerali Theophilus Yakubu Danjuma, akitokea Uganda alikokutana na Idi Amin, aliwasili Dar es Salaam Jumanne ya Novemba 14, 1978 na kukaa hadi Alhamisi ya Novemba 16.

Katika mazungumzo ya mjini Kampala, kwa mujibu wa jarida la Africa Research Bulletin, Idi Amin alimwambia Danjuma kuwa yuko tayari kuyaondoa majeshi yake mpakani iwapo tu OAU itamhakikishia kuwa Tanzania itasimamisha mapigano na “kuichokoza Uganda”.

Danjuma alikuwa na ujumbe kutoka kwa Rais wa Nigeria, Jenerali Olusegun Obasanjo kwenda kwa Mwalimu Nyerere ukimtaka kukubali mazungumzo na kusitisha mapigano.

Itaendelea kesho