Ofisi ya Mwanasheria Mkuu yazindua kamati ya ukaguzi wa ndani

Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali (wa pili kushoto), Dk Evaristo Longopa akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Kamati ya  Ukaguzi wa Ndani ya ofisi hiyo.

Muktasari:

  • Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG)imeanzisha kamati ya ukaguzi wa ndani yenye majukumu ya kufuatilia taarifa za fedha, utekelezaji wa masuala ya kisheria na masuala yanayohusu udanganyifu

Dodoma. Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeanzisha kamati ya ukaguzi wa ndani itakayokuwa ikifuatilia taarifa za fedha, utekelezaji wa masuala ya kisheria na udanganyifu.

Kamati hiyo imezinduliwa leo Desemba 12, 2018 na naibu mwanasheia mkuu wa Serikali, Dk Evaristo Longopa.

Amesema kamati hiyo ni jicho la pili katika kuishauri ofisi hiyo kama  inatekeleza majukumu yake  ipasavyo.

Dk Longopa amesema kamati hiyo ina wajibu wa kushauri kuhusu taarifa ya mwaka ya fedha  kujiridhisha na kumshauri ofisa masuhuli kabla ya taarifa hiyo haijawasilishwa kwa vyombo vinavyohusika.

Amesema jukumu jingine ni  kushauri kuhusu utekelezaji wa masuala mbalimbali ya kisheria yanayohusu menejimenti na udanganyifu.

Dk Longopa ameihakikishia kamati hiyo kutoingiliwa  katika utekelezaji wa majukumu yake.

Kamati hiyo ipo chini ya uenyekiti wa Waziri Kipacha kutoka sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, itatekeleza majukumu yake kwa  kipindi cha miaka mitatu.

“Unaweza ukadhani  unatekeleza majukumu yako ipasavyo kumbe siyo hivyo  kwa hiyo kamati  ya ukaguzi wa ndani ndio jicho la pili la kutuangalia kama tunakwenda sawa ama la,” amesema.

“Mnao wajibu na jukumu la kutushauri namna utendaji wa shughuli zetu unavyokwenda na niwaombe mtekeleze wajibu huo kwa uhuru kabisa.”

Amesema ofisi yake ambayo  hivi  karibuni imefanyiwa mabadiliko ya  kimuundo pia majukumu yake yameongezeka.