Pasipoti, Bendera ya Taifa vyazua balaa

Muktasari:

Matumizi ya Bendera ya Tanzania na Rangi zake,pamoja na Pasipoti bado vimeendelea kuwa gumzo nchini huku wadau mbalimbali wakitoa maoni tofauti.

Dar es Salaam. Wakati suala la matumizi ya bendera na wimbo wa Taifa yakiendelea kupasua vichwa vya watu nchini, suala la hati mpya za kusafiria linagonga vichwa kutokana na nukuu ya hotuba ya Baba wa Taifa, Julius Nyerere kukosewa.

Kwanza sehemu ya hotuba yake haijanukuliwa vizuri na pili tafsiri ya Kiingereza ina maneno yasiyo sahihi, huo ndio mjadala uliotanda kwa takriban siku tatu.

Hilo likiwa bado halijapoa, juzi, Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia iliwaandikia barua wakuu wa vyuo vya ualimu, vyuo vya ufundi na maendeleo ya jamii, vyuo vikuu na vishiriki na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo kuhusu matumizi sahihi ya rangi ya bendera na wimbo wa Taifa.

Wakati mjadala wa barua hiyo ukianza kupamba moto, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Joseph Mbele alitumia mtandao wa Facebook kuibua makosa katika hati ya kusafirikia. Na yeye pia akaibua mjadala mzito.

Katika barua hiyo ya wizara iliyosambaa mitandaoni inaeleza kuwa imepokea maelekezo kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani, kuhusu makosa katika matumizi ya alama hizo za Taifa.

“Kutokana na makosa hayo Wizara ya Mambo ya Ndani inaelekeza kuwa wimbo wa Taifa utapigwa kwenye dhifa za kitaifa, endapo hadhi ya sherehe haitambuliki, taasisi italazimika kuomba kibali kwa waziri mwenye dhamana,” inaeleza barua hiyo.

“Wimbo unatakiwa kuimbwa kwa ukamilifu beti zote mbili kwa kuzingatia nota na maneno.”

Pia ilizungumzia rangi za Bendera ya Taifa.

“Rangi za Bendera ya Taifa ni kijani, dhahabu, nyeusi na bluu. Ni makosa kutumia rangi ya njano na uwiano wa bendera ni 2/3 katika urefu na upana.”

Mwananchi ilipozungumza na katibu mkuu wa Wizara ya Elimu, Dk Leonard Akwilapo kuhusu suala hilo, alisema: “Unataka ufafanuzi gani? Kwani barua umeandikiwa wewe. Ungekuwa umelengwa wewe ningekupa ufafanuzi lakini sio. Walioandikiwa wanaelewa zaidi. Sasa sijui unataka ufafanuzi gani.”

Lakini mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Dk Benson Bana alishangazwa na maagizo hayo akisema kuzuia kuzitumia alama hizo ni kuua uzalendo.

Alisema pamoja na kuwapo kwa matakwa ya kisheria, utekeklezaji wake huenda ukawafanya watu wasione umuhimu wa alama hizo au kuzihofia kwa kuwa zitawanyima uhuru wa kuzitumia.

“Hivi kuna tatizo gani na Bendera ya Taifa? Kwa mfano Mimi kama ni mwalimu wa uraia huwa ninafarijika sana ninapoona watu wanatembea na bendera yao, hata kama haikidhi matakwa ya kisheria,” alisema.

“Hizi alama za taifa ni muhimu katika kukuza uzalendo, hata Waziri Kangi Lugola anatembea na shati lenye bendera. Sidhani kuna sheria inaruhusu lakini sisi tulimuona ni mzalendo tu.”

Kuhusu wimbo wa Taifa, Dk Bana alisema nalo ni suala mtambuka kwa kuwa hata anayestahili kutoa kibali hafahamiki.

“Ukaombe kibali kwa nani? Shughuli yoyote ya kiserikali au kijamii kuimba wimbo wa Taifa ni jambo jema,” alisema.

Alishauri watendaji wa Serikali kutilia mkazo masuala ya msingi kama kuboresha elimu badala ya kutumia muda mwingi kwenye mambo yasiyo na tija.

Makosa katika hati ya kusafiria pia limekuwa na mjadala mkubwa

Maneno yaliyoibua mjadala ni nukuu ya hotuba ya Mwalimu Nyerere ya Desemba 9, 1961, isemayo “Sisi tumekwishauwasha mwenge wa uhuru na tumeuweka juu ya Mlima Kilimanjaro. Umulike ndani na nje ya mipaka yetu, ulete tumaini pale ambapo hakuna matumaini, ulete upendo mahali penye chuki na heshima palipojaa dharau.”

Kosa linaloonekana ukurasa wa 47 ni kushindwa kutofautisha nyakati kati ya ‘tumeweka’ badala ya ’tuliuweka’.

Profesa Mbele alisema makosa hayo ni aibu kwa Taifa na kushauri kutengeneza upya hati hiyo.

“Kifupi pasipoti hizi mpya zinatakiwa kutengenezwa upya hata kama itagharimu kiasi kikubwa cha fedha,” aliandika.

Alipoulizwa na mwandishi wa The Citizen, ofisa mawasiliano wa Idara ya Uhamiaji, Ally Mtanda alisema bado hawana taaarifa ya suala hilo.

“Bado hatujakutana na malalamiko kama hayo. Tafadhari nitumie ili niweze kuwasilisha kwa mabosi kabla ya kuizungumzia baadaye,” alisema.

Alipotafutwa tena alisema amewasilisha suala hilo, lakini hakulitolea ufafanuzi.

Na jana simu yake na ya Naibu Waziri Mambo ya Ndani, Hamad Masauni hazikuwa zinapokelewa.