Polepole atajwa kushuka mapato

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole

Muktasari:

Katibu huyo wa uenezi wa CCM anahusishwa na kushuka kwa mapato ya manispaa hiyo baada ya kutoa maelekezo yanayodaiwa kukinzana na uamuzi wa madiwani walioutoa katika kikao cha baraza lao

Kigoma. Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Mwailwa Pangani amesema kitendo cha Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole kuingilia mgogoro kati ya manispaa hiyo na wafanyabiashara kimesababisha kushuka kwa mapato yaliyopitishwa na baraza la madiwani.

Polepole alifanya ziara mkoani Kigoma mwezi Machi ambapo pamoja na mambo mengine alisikiliza kero za wafanyabiashara wa masoko yaliyopo Manispaa ya Kigoma Ujiji waliokuwa wakilalamikia kupanda kwa tozo za vizimba kutoka Sh15,000 hadi Sh50,000.

Akizungumza hivi karibuni na mwandishi wa habari hizi jijini Dar es Salaam, Polepole alikiri kuingilia mzozo huo.

“Ni kweli huo mgogoro naujua. Chama kinapokuwa madarakani ndicho kinachotawala, hata ukienda Marekani, Republican ya Trump (Donald-Rais wa Marekani) ndiyo inayotawala Serikali. Lakini pale (Ujiji) kuna madiwani wanafikiri wana Serikali yao,” alisema Polepole.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa manispaa hiyo, Pangani alipozungumza na Mwananchi mjini Kigoma, alisema kiwango hicho kilipitishwa na baraza la madiwani kwa kufuata sheria ya utungaji wa sheria ndogo na kuwashirikisha wanachi. “Siyo kwamba hatujashirikisha wananchi, unajua Watanzania kusoma matangazo huwa ni tatizo. Kwa sababu kuandaa by law (sheria ndogo) inaanzia halmashauri na kabla haijaenda kwenye baraza inakwenda kwenye kata na rasimu zinawekwa kwenye matangazo ili mwananchi mwenye pingamizi atoe kwa siku 21,” alisema mkurugenzi huyo.

“Kwa hiyo ukikaa siku 21 haujapata pingamizi inawezekana wananchi wengi hawasomi, inapita. Ndiyo sheria inavyosema.”

Alisema kutopandishwa kwa ushuru huo kumesababisha manispaa hiyo kuambulia asilimia 52 ya mapato tofauti na matarajio ya kufikia asilimia 100.

Alisema hata asilimia hiyo wameipata baada ya Ofisi ya Rais (Tamisemi) kutoa waraka ulioweka kiwango cha Sh25,000.

“Halmashauri ilipanga Sh50,000 kwa kila chumba, wananchi wakagoma. Kesi ikaenda mahakamani, lakini Serikali ikaingilia kati kutoa suluhisho kwamba wafanyabiashara watoe Sh25,000 kwa kila chumba,” alisema Pangani.

Alisema mgogoro huo ulidumu kwa miezi sita ambayo manispaa haikukusanya chochote kutoka kwenye masoko na hatimaye kuagizwa kutoza Sh25,000.

“Yeye (Polepole) alisema hiyo hela ni nyingi na wakati huo wananchi walishafungua kesi mahakamani. Itatuathiri lakini ni afadhali kupata hiyo kuliko wakati ule hatukupata kitu.”

Akifafanua zaidi, Meya wa manispaa hiyo, Hussein Ruhava alisema walianzisha juhudi za ukusanyaji wa mapato 2016/17 ili kuongeza mapato.

“Kwa hiyo tukapandisha bajeti kufikia Sh2.4 bilioni kutoka Sh2.01 bilioni iliyokuwepo awali. Sehemu kubwa tuliyoiwekea mikakati ni idara ya mipango miji hususan kodi za majengo ambako tulilenga kupata Sh1.1 bilioni. Lengo lilikuwa ni kuboresha miundombinu ya wananchi,” alisema Ruhava.

Hata hivyo, alisema yalitokea mabadiliko ya Serikali kwa kuchukua vyanzo vya kodi ya majengo.

Kutokana na mabadiliko hayo, alisema waliamua kujielekeza kwenye masoko ambayo awali walitoza Sh15,000 kwa kila chumba cha biashara kwa mwezi.

“Kwa hiyo, baraza likatoa mapendekezo na kutunga sheria ndogo ili kukusanya Sh50,000 katika masoko hasa ya Mwanga na Kigoma na masoko mengine Sh15,000, 20,000 na 30,000,” alisema.

Alisema kutokana na mapendekezo hayo walikusudia kukusanya zaidi ya Sh1 bilioni na uamuzi ulipitishwa na madiwani. Hata hivyo alisema malengo hayakufikiwa hivyo waliishia kupata Sh1.4 bilioni kutoka kwenye vyanzo vingine.

“Kwa hiyo utaona kuna Sh1.4 bilioni ambazo tumezisoma kwenye ripoti ya makusanyo, ukiondoa chanzo cha kodi ya majengo basi tungekusanya zaidi ya asilimia 100,” alisema Ruhava.

Baadhi ya madiwani waliokuwa katika mkutano mkuu wa manispaa hiyo hivi karibuni walielekeza lawama zao kwa Polepole wakisema alitia chumvi kwenye mgogoro huo na kuisababishia hasara manispaa.

Diwani wa Rubuga (Chadema), Omari Gindi alisema mgogoro huo ndiyo ulikuwa sababu ya kupata hati chafu katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mwaka 2016/17.

“Tulipitisha makadirio hayo Februari, Machi akaja Polepole akatuvuruga, akaondoka. Kimsingi hana nafasi katika utendaji wa Serikali lakini watumishi wa umma wanamwogopa sana,” alisema.

Diwani wa Kipampa (ACT Wazalendo), Mussa Ngongolwa alisema kodi waliyoipitisha ilikuwa ya kisheria, lakini iliingiliwa na siasa.

“Ni masuala ya siasa na hayapo kiutaratibu na ni kosa na imesababisha tupate hati chafu kwa sababu makusanyo yalikuwa chini ya kiwango, hatukukusanya kama tulivyotarajia,” alisema.

Diwani wa viti maalumu (CCM), Mgeni Kakuru alisema, “(Polepole)alipofika hapa alipokea malalamiko ya wafanyabiashara. Akamwagiza mkurugenzi afanye vikao na wafanyabishara ili tukubaliane.”

Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Kigoma Ujiji, Juma Chaurembo alisema Polepole aliingilia mgogoro huo baada ya kumuomba

“Sio kwamba wafanyabiashara wote ni CCM, ila tunapoona mahali kuna suluhisho lazima tuingie. CCM ni chama tawala kinaweza kutoa maagizo kwa Serikali,” alisema.

Ofisi ya CAG imeipa manispaa hiyo hati chafu kwa miaka mitatu mfululizo.