Polisi Mtwara watoa kauli kujinyonga mfanyabiashara wa korosho

Muktasari:

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara limesema linaendelea na uchunguzi wa kifo cha Moses Wadasan (35) mkazi wa Dodoma aliyejinyonga hadi kufa Desemba 16, 2018 eneo la Maduka Makubwa mkoani humo


Mtwara. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara limesema linaendelea na uchunguzi wa kifo cha Moses Wadasan (35) mkazi wa Dodoma aliyejinyonga hadi kufa Desemba 16, 2018 eneo la Maduka Makubwa mkoani humo.

Taarifa iliyotolewa leo Jumanne Desemba 18, 2018 na kamanda wa polisi mkoani humo, Blasius Chatanda  inaeleza kuwa Wadasan alijinyonga kwa kutumia waya na mwili wake kukutwa unaning’inia juu ya mti.

Amesema marehemu alikuwa Mtwara kutafuta shughuli za uchukuzi wa korosho ambazo huzifanya kila mwaka katika msimu wa korosho.

“Baada ya kupata taarifa timu ya makachero ilifika na kufanya ukaguzi eneo la tukio kisha kuuchukua mwili hadi hospitali ya Rufaa Ligula kwa uchunguzi zaidi,” inaeleza taarifa hiyo.

Inaeleza  kuwa taarifa kutoka kwa ndugu wa marehemu zinaeleza kuwa alichukua uamuzi huo kutokana na maradhi ya mara kwa mara yaliyokuwa yakimsumbua.

“Hata hivyo uchunguzi wa daktari utatupa majibu kama alikuwa na maradhi yanayoelezwa,” imefafanua taarifa hiyo.