Precision walia hasara kugonga ndege Mwanza

Muktasari:

  • Takwimu zinaonyesha katika kipindi cha mwaka 2011-2014 kulikuwa na takriban matukio 67,000 ya namna hiyo duniani kote kwa ndege kuvamiwa na ndege viumbe.

Dar es Salaam. Shirika la Ndege la Precision Air limelazimika kulipia gharama za matengenezo kutokana na tukio la Desemba 9 la ndege yake kuvamia na viumbe wakati ikitua Mwanza.

Ndege wamekuwa tatizo Uwanja wa Kimataifa wa Mwanza kutokana na kuwepo kwa wingi na kuingia kwenye injini za ndege wa abiria wakati zikitua au kupaa.

Uvamizi wa viumbe hao kwenye ndege, ulisababisha Precison Air kusitisha au kubadili muda wa safari kwa abiria wao, ingawa tayari imerejesha huduma za kawaida.

Ofisa uhusiano wa kampuni ya Precision Air, Hilary Mremi alisema tukio hilo limesababisha hasara kwa kampuni hiyo kutokana na kulazimika kuchunguza ndege yao na kuwatafutia abiria usafiri mwingine na kulipia malazi yao.

“Matukio ya namna hii huwa yanatokea lakini la kwetu lilikuwa baya zaidi. Nadhani ndege hao wanaweza kudhibitiwa wasiwe kwenye runway (barabara inayotumiwa na ndege kupaa au kutua),” alisema Mremi.

“Kama wakulima wa mpunga wanaweza, viwanja vya ndege haishindikani.”

Mapema wiki hii zilisambaa picha zinazoonyesha damu za ndege hao zikiwa zimetapakaa mbele ya ndege. Ilieleezwa kuwa ndege hiyo ni ya Shirika la Tanzania (ATCL) na tukio hilo lilitokea Mwanza.

“Tukio la kwetu ni dogo na la kawaida, halikuwa na athari zozote kama lile la Precision ambalo hata sisi kama wadau wa usafiri wa anga lilitusikitisha,” alisema Josephat Kagirwa, mkuu wa kitengo cha mawasiliano cha ATCL.

“Ndege kuwepo eneo kama lile lililopo kando ya ziwa ni kawaida.”

Wakati lilipotokea tukio la ndege ya Precision, mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya usimamizi wa viwanja vya ndege (TAA) Richard Mayogela alisema tayari ametuma timu maalumu kushughulikia tatizo hilo.

“Kuna kamati inayojumuisha vijana ambao wamekuwa wakishiriki kudhibiti ndege hao. Nadhani katika matukio ya hivi karibuni hawakuwa uwanjani kusaidia,” alisema Mayogela.

Alisema mpaka sasa ameshaagiza timu ya watu kadhaa kushughulikia jambo hilo na kwamba Serikali itajifunza kutoka kwa nchi ambazo zina matatizo kama hayo, lakini pia matumizi ya teknolojia kufukuza ndege hao.

Aidha tukio hilo sio jipya.

Mwaka 2016, shirika la Fast Jet lililazimika kupangua ratiba za huduma zake baada ya ndege hao kuvamia injini ya moja ya ndege zake kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Mwanza.

Wakati huo, Naibu Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, Edwin Ngonyani alisema tatizo la ndege hao linatokana na uwanja huo kuwa karibu na soko la samaki.

Alisema wavuvi wana tabia ya kutupa ovyo masalia ya samaki, hali inayosababisha ndege wengi kwenda eneo hilo kujipatia chakula na hivyo kuathiri shughuli za uwanja wa ndege.

Shambulio la ndege hao lilikuwa kipindi kama cha sasa cha Desemba.

Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la matukio hayo. Mwaka 2016, Uingereza pekee iliwahi kukumbwa na matukio 1,835 kama hayo.

Takwimu nyingine zinaonyesha kuwa katika kipindi cha mwaka 2011-2014 kulikuwa na takriban matukio 67,000 ya namna hiyo duniani kote na inaelezwa kuwa kiwango cha msafara wa ndege kuvamia wa ndege kimekuwa kikiongezeka kwa wastani wa asilimia 10.

Ingawa matukio mengi hayajawahi kuhusisha na ndege kuanguka, lakini mashirika mengi yamekuwa yakiingia hasara kutokana na uharibifu.

Kati ya viwanja vya ndege vinavyoonekana kufanikiwa kudhibiti uvamizi huo ni Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Edmonton, Canada ambao unatumia teknolojia ya robirds, yaani ndege wa bandia kudhibiti viumbe hao.

Robirds ni ndege anayerushwa kwa kutumia kifaa maalumu, Huweza kuruka mbali na kwenda kasi mithili ya tai, ambaye huogopwa na ndege wadogo na hivyo kila wakati viumbe hao wanapojaa, hurushwa eneo hilo na kusababisha ndege halisi kukimbia.

Njia nyingine ni kudhibiti mazalia ya ndege kwenye maeneo ya uwanja, hasa majengo na katika baadhi ya sehemu kelele hutumika kuwafanya ndege wasiishi kwa raha.

Katika sehemu hizo, kifaa maalumu mithili ya bastola huwekwa baruti ambayo hufyatuliwa na kwenda kulipukia hewani na hivyo kufukuza ndege, kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Habari la Uingereza (BBC) ya mwaka 2013.

Mara nyingi ndege zinazokumbwa na matukio kama hayo marubani wake wanachukua uamuzi wa haraka wa kutua kwa dharura katika viwanja jirani na kuwabadilishia abiria ndege katika ndege nyingine.

Akizungumza na Mwananchi, meneja wa Uwanja wa Mwanza, Maulid Mohamed alisema kwa sasa wanawafukuza viumbe hao kwa kutumia magari maalumu.

Alisema kuna watu maalum wamewekwa ili kuwafukuza viumbe hao na kuhakikisha hawapo wakati ndege inapotua. Watu hao hutumia ishara kutoka kwa muelekezaji uwanjani hapo.

“Tumeandaa huu mkakati wa kuwatumia watu na magari ili waweze kuwahangaisha wakati ndege inapokaribia kutua,” alisema.