Profesa Mzumbe alalamikia tatizo la ajira kukosa kipaumbele

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda (mwenye koti) akisalimiana na mkuu wa chuo kikuu mzumbe Jaji mstaafu Barnabas Samatta baada ya kumalizika kwa mahafali ya 17 ya chuo yaliyofanyika kampasi kuu Morogoro. Picha Hamida Shariff

Muktasari:

  • Wahitimu 2,533  katika Chuo Kikuu cha Mzumbe  wametunukiwa shahada za umahiri, shahada, stashahada na astashahada katika mahafali ya 17 ya chuo hicho leo

Morogoro. Changamoto ya ajira kwa wahitimu wa vyuo vikuu bado haijapewa kipaumbele na hiyo inatokana na kukosekana kwa takwimu sahihi za wahitimu wanaokosa ajira na walioko kwenye ajira isiyokuwa rasmi ambayo hawakuisomea.

Hayo yameelezwa leo na mwenyekiti wa baraza la Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa Methew Luhanga wakati wa mahafali ya 17 ya wahitimu wa kozi mbalimbali waliohitimu chuoni hapo.

Profesa Luhanga amesema pamoja na changamoto hiyo wahitimu hao wanatakiwa kuwa chachu ya maendeleo hasa katika kuhakikisha nchi inakuwa ya uchumi wa viwanda.

Aidha, amewataka wahitimu watakaofanikiwa kuajiriwa katika sekta mbalimbali zikiwAmo za Serikali kujiepusha na vitendo vya ufisadi na uvivu badala yake walitumikie taifa kwa uadilifu na uaminifu mkubwa.

Awali, mhadhili mwandamizi wa chuo hicho, Profesa Cyriacus Binamungu aliwataka wahitimu hao kujiendeleza kitaaluma na kutokatishwa tamaa na changamoto mbalimbali zikiwamo za kukosa ajira.

“Soko la ajira litawatambua ninyi kama wasomi kutokana na matendo yenu baada ya kuhitimu na mfahamu kwamba kuhitimu sio kuvaa joho na kupata cheti bali ni kuitumia taaluma mliyoipata katika kutatua changamoto kwenye jamii,” alisema Profesa Binamungu.

Naye Makamu mkuu wa chuo hicho, Profesa Lugano Kusiluka alisema baadhi ya wahitimu hao ambao walikuwa wakisoma kupitia mikopo wamekuwa wakifanya vizuri na hivyo ameishauri Serikali kuendelea kuwekeza kwenye taasisi za elimu ya juu ili kupata wataalamu.

Alisema ili kufikia kwenye uchumi wa kati unaotokana na viwanda lazima taasisi za elimu ya juu zishirikiane na sio kushindana.

Katika mahafali hayo ambayo pia yalihudhuriwa na mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda, Jaji mstaafu Barnabas Samatta aliwatunukia wahitimu 2,533 shahada za umahiri, shahada, stashahada na astashahada.