Quality Centre ya Manji hatarini kufilisiwa

Muktasari:

Mali za mfanyabiashara maarufuTanzania, Yusuf Manji ni pamoja na jengo maarufu jijini Dar es Salaam lijulikanalo kwa jina la Quality Centre.

Dar es Salaam. Mali za mfanyabiashara maarufu nchini, Yusuf Manji zenye thamani ya mabilioni ya shilingi ziko hatarini kufilisiwa baada ya kuwekwa chini ya wadhibiti na wakabidhi wasii ili kulipa madeni makubwa yanayodaiwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki na Kusini.

Mali hizo ni pamoja na jengo maarufu jijini Dar es Salaam lijulikanalo kwa jina la Quality Centre.

Taarifa zilizotolewa jana na wafisili na wakabidhi wasii hao chini ya Kampuni ya Price Water House Coopers (PWC), ilisema kuanzia jana, Manji hataruhusiwa kumiliki mali hizo hadi atakapolipa madeni hayo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo mameneja wanaosimamia kazi hiyo, David Tarimo na Nelson Msuya wameteuliwa na benki hiyo ili kukamilisha kazi ya ukusanyaji wa madeni na ikishindikana mali hizo zitapigwa mnada.

Hata hivyo, alipoulizwa na Mwananchi madeni anayodaiwa Manji na benki hiyo, Tarimo wa PWC alisema hawezi kutaja kwa kuwa itakuwa ni kwenda kinyume na maadili ya kazi yao.

Jengo la Quality Centre lililojengwa zaidi ya miaka 10 iliyopita liko katika kiwanja Na.25 kandokando ya Barabara ya Nyerere (zamani Pugu Road) na katika miaka ya hivi karibuni, limekuwa kivutio kikubwa cha watalii wa ndani na nje ya Jiji la Dar es Salaam kutokana na shughuli za kiuchumi zinazofanyika hapo.

Taarifa zinaeleza kuwa hata mali zilizomo ndani ya jengo hilo zinazomilikiwa na Quality Group Limited nazo zinashikiliwa.

Kwa mujibu wa taarifa za kisheria zilizotolewa na wafilisi na wakabidhi wasii hao zimesema wanayo dhamana ya kumiliki hati za mali zinazohamishika na zisizohamishika ili kurejesha madeni anayodaiwa mfanyabiashara huyo na benki iliyotajwa hapo juu kama mdeni atashindwa kulipa.

Mfumo wa ukabidhi mali chini ya ufilisi kwa mujibu wa wanasheria, ni mchakato wa kumteua mwangalizi wa mali kwa muda ulioainishwa hadi kazi ya kurejesha madeni inapokamilika au wale wanaodaiwa kulipa au mali kununuliwa na mwekezaji mwingine.

Wataalamu wa sheria pia wanasema watu wenye madaraka ya kusimamia mchakato huo ni mahakama ambayo ina nguvu kisheria, kampuni yenye mamlaka ya kisheria au wanasheria waliopewa mamlaka yanayolingana na taasisi hizo.

“Katika zoezi hili pia tuna dhamana ya kumiliki hisa za mali na kuiongoza kampuni na mali zote zilizoko chini ya mashtaka kwa ajili ya kulipa madeni yanayodaiwa na benki,” wanasema wasimamizi hao.