RC Dodoma ataka Tarura kutekeleza ahadi za JPM

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge ameutaka Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) kutekeleza ahadi za ujenzi wa barabara zilizotolewa na Rais John Magufuli

Dodoma. Wakala wa barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) wametakiwa kukamilisha ahadi za ujenzi wa barabara zilizotolewa na Rais John Magufuli ili wananchi wasione kuwa kiongozi mkuu huyo wa nchi ameahidi na kushindwa kutekeleza.

Hayo yameelezwa leo Jumatatu Desemba 17, 2018 na mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge kwenye kikao cha bodi ya barabara.

Amesema utekelezaji  wa ahadi hizo ni muhimu kwa sababu ziliahidiwa na mkuu wa nchi.

Dk Mahenge amesema pamoja na utekelezaji wa barabara hizo kuanza umuhimu wa kukamilisha barabara hizo kwa kuwa zinaunganisha maeneo makubwa ya halmashauri na wilaya.

“Naiomba Tarura wazipe kipaumbele ahadi zote za ujenzi wa barabara zilizotolewa na Rais pamoja na viongozi wakuu wa nchi  Ili zikamilike kwa wakati. Wasipofanya hivyo wananchi wataona kuwa Rais aliwaahidi lakini hakutekeleza kitu ambacho hakipendezi," amesema.

“Pamoja na utekelezaji wa ahadi hizo za Rais pia Tarura wanatakiwa kushirikiana na viongozi wa halmashauri hasa mkurugenzi ili kujua vipaumbele vya ujenzi wa barabara zilizopo kwenye halmashauri zao kuliko kufanya kazi bila kushirikiana."

Kwa upande wake Salome Kabunda kutoka Wakala wa Barabara (Tanroads) amesema barabara nyingi zilizoahidiwa na Rais zinajengwa, nyingi zimekamilika na kukabidhiwa serikalini huku chache zikiwa katika hatua mbalimbali.

Amesema mwaka 2018/19, wakala huo ulitengewa Sh19bilioni kwa ajili ya ujenzi wa barabara, madaraja  na barabara kuu mkoani Dodoma.