RC Hapi: Meya Kimbe amekamatwa na Takukuru akipokea rushwa

Meya wa Manispaa ya Iringa, Alex Kimbe

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi leo Ijumaa amezungumza na waandishi wa habari ofisini kwake ambapo amesema Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) inamshikilia Meya wa Manispaa ya Iringa, Alex Kimbe

Iringa. Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi amesema Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani humo, inamshikilia Meya wa Manispaa ya Iringa, Alex Kimbe kwa tuhuma za kupokea rushwa kutoka kwa mzabuni anayekusanya ushuru wa  manispaa hiyo.

Akizungumza leo Ijumaa Novemba 16, 2018, Hapi amesema Kimbe amekamatwa akiwa anapokea rushwa jana majira ya saa 11 kuelekea saa 12 jioni katika Hoteli ya Gentle Hill kutoka kwa mzabuni ambaye amepewa kazi ya kukusanya ushuru.

Amesema Takukuru imekuwa ikifanya uchunguzi na kugundua kuna watumishi ambao wanapokea rushwa kutoka kwa wananchi na wazabuni mbalimbali.

"Meya amekamatwa jana na Takukuru akiwa katika Hoteli ya Gentle Hills akipokea rushwa kutoka kwa mkurugenzi wa kampuni ya Gracious kwa madai alimuahidi kumpa tenda ya kukusanya ushuru na ujenzi mkoani hapa,” amesema.

“Hivyo, baada ya kufuatilia Takukuru walimkamata na sasa anashikiliwa na baada ya kukamilika kwa taratibu atafikishwa mahakamani," amesema Hapi.

Hapi amesema kumekuwepo na tuhuma kadhaa za rushwa katika halmashauri za mkoa wa Iringa ziko zinazohusu viwanja, wananchi wanalalamika madiwani wanajigawia viwanja kinyume na sheria.

"Wananchi wanalalamika kunyimwa vibali vya ujenzi mpaka watoe rushwa, kuna tuhuma za utoaji zabuni kwa misingi ya rushwa na upendeleo jambo ambalo Takukuru imefanya uchunguzi na kufanikiwa kumkamata meya," amesema Hapi.

Hapi amewaonya watendaji viongozi na watumishi wa umma wajiepushe na vitendo vya rushwa na kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni za maadili ya utumishi wa umma.