RC alia Dodoma kutofanya vizuri katika elimu kitaifa

Muktasari:

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge amesema mkoa huo uko nyuma kielimu kufuatia matokeo ya mitihani ya kitaifa yaliyotangazwa hivi karibuni


Dodoma. Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge amesema mkoa huo uko nyuma kielimu kufuatia matokeo ya mitihani ya kitaifa yaliyotangazwa hivi karibuni.

Amesema mwaka 2018 Dodoma imepanda kutoka asilimia 63 ya ufaulu  hadi 70 na kwa upande wa nafasi za kitaifa imeshika nafasi ya 24 mwaka 2017 na 23 mwaka 2018.

Akizungumza leo Desemba 18 2018  jijini Dodoma katika kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa (RCC),  amewataka watendaji wote kuanzia ngazi za chini kuchukua hatua za kuuinua mkoa huo kielimu.

Amesema hali ni mbaya kuanzia mahudhurio ya watoto waliochaguliwa, akibainisha kuwa waliopo shuleni wanaonekana kuzagaa mitaani huku wenzao wakiwa darasani.

"Unaweza kuona kuwa tumefaulu vizuri kutoka asilimia 63 hadi asilimia 70 lakini tumekuwa wa 23 tumepanda kwa nafasi moja kutoka 24 sasa hao wenzetu wanaokuwa namba moja wakoje wanatuzidi nini,” amehoji.