VIDEO: Rayvanny, Diamond walipishwa mamilioni kisa wimbo Mwanza

Muktasari:

Kila mmoja ametakiwa kulipa faini ya Sh3 milioni kwa kutoa wimbo huo ikidaiwa unakiuka maadili

Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) limewatoza Sh9 milioni wanamuziki Rayvanny na Diamond Platnumz , kwa kutoa wimbo Mwanza ikieleza kuwa una mashairi yanayokiuka maadili.

Hatua hiyo imekuja baada ya leo Novemba 13 kufanyika kikao kati Rayvanny ambaye ndiye mwenye wimbo huo, kilichoketi kwa takribani saa tatu katika ofisi za Baraza hilo zilizopo Ilala Bungoni, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu wa Baraza hilo, Godfrey Mngereza amesema kiasi hicho cha fedha kimetozwa kwa wasanii Rayvany na Diamond kila mmoja  Sh3 milioni na kwa lebo ya Wasafi ambayo nayo imesajiliwa Basata.

Sambamba na hilo, Mngereza amesema wametakiwa kupeleka mashairi ya wimbo huo na kusisitiza kuwa hakuna mahala utakaporuhusiwa kupigwa hapa nchini Tanzania iwe usiku au mchana kwa kuwa hauifai.

“Huu wimbo haufai kabisa. Hata kwenye kikao tumemuuliza Rayvanny je, unaweza kuuimba mbele ya wazazi wako akajibu hapana, inaonyesha namna gani hata yeye anaona hauna maadili, na kwa nini tupige marufuku usipigwe halafu turuhusu ifanywe hivyo usiku?" Alihoji Mngereza.

Kwa upande wake Meneja wa lebo ya Wasafi, Hamis Taletale 'Babu Tale'  amesema katika kikao yameamuliwa mambo mawili ikiwamo kupeleka mashairi ya wimbo huo yakahaririwe na kutoendelea kuusambaza.

Akizungumza mara baada ya kikao hicho kilichodumu kwa takribani saa tatu, Babu Tale amesema barua ya kuitwa kikaoni waliipata jana jioni na kati ya mambo waliokubaliana ni kupeleka mashairi ya wimbo huo.

Kuhusu kuufuta kwenye mitandao amesema hilo wataenda kulijibu kwa barua.

Suala la wasanii wao kujitetea kupitia Instagram, amesema wameona mambo yatakayozungumzwa kikaoni huenda yakabaki humo, hivyo wameamua kutumia majukwaa ya mitandao kueleza utetezi wao.